Buhari: Naendelea kupata nafuu

Rais Muhammadu Buhari na mkewe
Maelezo ya picha,

Rais Muhammadu Buhari na mkewe

Rais wa Nigeria anayeugua Muhammadu Buhari amemuandikia mwenzake wa Guinea Alpha Conde kumshukuru kwa maombi ya kitaifa aliyopanga ili kumwezesha kupona, kulingana na msemaji wake Femi Adesina.

Bwana Buhari mwenye umri wa miaka 74 amekuwa nchini Uingereza kwa takriban siku 80 akipata matibabu kwa ugonjwa usiojulikana.

Katika barua yake ,bwana Buhari alimuhakikishia bwana Conde ambaye ndio mwenye kiti wa muungano wa Afrika kwamba alikuwa anaendelea kupona na kwamba atarudi nchini Nigeria ili kuendelea na huduma zake mara moja atakapoambiwa na daktari wake, aliongezea Adesina.

Katika barua ya mapema ,bwana Buhari alikuwa amekubali uteuzi wake kama kiongozi wa AU 2018 ajenda kuu ikiwa vita dhidi ya ufisadi , alisema bwana Adesina.

''Ningependa kusema kwamba nimekubali jukumu hili jipya na kusisitiza juhudi zangu za kuchangia juhudi zetu kuimarisha utawala bora na maendeleo barani'', Buhari alisema katika barua.

Alichaguliwa kuchukua wadhfa huo katika mkutano wa AU mjini Ethiopia mnamo mwezi Julai 4.

Kutokuwepo kwa Bwana Buhari kumezua wasiwasi nchini Nigeria na kuzua uvumi kwamba wapinzani wake walikuwa wanapanga kumrithi.