Kiongozi wa Mai-Mai Sheka ajisalimisha DRC

DRC

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Ntabo Ntaberi Sheka akizungumza

Mmoja miongoni mwa wapiganaji wa vita maarufu sana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amejisalimisha kwa walinda amani wa umoja wa mataifa.

Kikosi maalumu cha kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kimemtaja Ntabo Ntaberi Sheka, na kumwelezea kuwa ndiye kiongozi mkuu wa kijeshi wa kundi lililokuwa likijulikana kama Mai-Mai Sheka, alimua kujisalimisha karibu na ngome yake mashariki mwa Kongo.

Baada ya kujisalimisha hatua inayofuata ambayo inamhusu ni kukabidhiwa kwa serikali ya nchi hiyo, ambayo miaka sita iliyopita ilitoa hati ya kukamatwa kwake kwa madai na makosa ya Uhalifu dhidi ya ubinadamu na Uhalifu wa vita.

Kundi hilo la Mai-Mai Sheka linatuhumiwa pia kwa makosa ya ubakaji na pia kuwatendea ukatili wa kutisha na kuwaacha wafe taratibu raia wa nchi hiyo

Shirika la kutetea haki za binaadamu lililoko mjini New York limetoa rai kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumtendea mtuhumiwa huyo ubinaadamu wakati wote wa kesi yake na kwamba haki zake kama binaadamu zisikiukwe.