Wataka Machar ashirikishwe mazungumzo ya amani Sudan K

Riek Machar
Maelezo ya picha,

Riek Machar

Wanaharakati wa kijamii nchini Sudan Kusini wanasema kuwa hatua ya kumtenga kiongozi wa waasi aliye mafichoni Riek Machar kutoka kwa mpango mpya wa amani utaongeza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Wamesema kuwa iwapo amani itaimarishwa pande husika katika mgogoro huo ni sharti zishirikishwe.

Mawaziri kutoka mataifa ya Afrika Mshariki ,wanaokutana nchini Sudan Kusini wiki hii walisema kuwa wawakilishi wa Machar wataalikwa.

Lakini yeye mwenyewe hataalikwa.

Mamilioni ya raia wametoroka makwao tangu vita vizuke baada ya rais Salva Kiir kumfuta kazi makamu wake Riek Machar .

Miaka miwili kabla ya vita hivyo taifa hilo lenye idadi kubwa ya Wakristo lilikuwa limekuwa taifa jipya duniani baada ya kujitenga na Sudan lenye Waislamu wengi.