Gari la Justin Bieber lamgonga mpiga picha

Gari la Justin Bieber lilimgonga mtu aliyetajwa kuwa mpiga picha

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Gari la Justin Bieber lilimgonga mtu

Justin Bieber amehusika katika ajali iliofanyika eneo la Beverly Hills, maafisa wa polisi wamethibitisha kwa BBC.

Kanda ya video imeonyesha mwanamuziki huyo akimgonga mtu aliekuwa akitembea kwa miguu baada ya kutoka katika ibada ndani ya kanisa moja mjini Los Angeles siku ya Jumatano.

Idara ya polisi mjini Beverly Hills imesema kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa polepole wakati wa ajali hiyo.

Maafisa wa polisi wa eneo la Beverly Hills waliwasili katika eneo la ajali hiyo na kumpata mwanamume mmoja ambaye alikuwa amelala chini.

Alisafirishwa hadi hospitalini bila majeraha hatari.

Bieber alisalia katika eneo hilo la ajali kushirikiana na maafisa wa polisi na baadaye akaachiliwa.

Bieber alionekana amesimama na kuzungumza na mtu aliyejeruhiwa ambaye alidaiwa kuwa mpiga picha baada ya kisa hicho.

Sajenti Stout alithibitisha kwamba Bieber alitoka nje ya gari lake na kujaribu kumpatia huduma ya kwanza baada ya ajali hiyo.