Vita vyasababisha watoto 850,000 kukosa makao DR Congo

Watoto wengi walioathiriwa kwa sasa wako chini ya usimamizi wa jamaa zao.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Watoto wengi walioathiriwa kwa sasa wako chini ya usimamizi wa jamaa zao.

Takriban watoto 850,000 wamelazimika kutoroka vita katika mkoa wa Kasai nchini DR Congo kulingana na maafisa wa Unicef.

Idadi hiyo ndio imetajwa kuwa kubwa zaidi kulingana na ripoti hiyo.

Watoto wengi walioathiriwa kwa sasa wako chini ya usimamizi wa jamaa zao.

Vita vilizuka huko Kasai mnamo mwezi Agosti 2016 baada ya kiongozi mmoja wa kitamaduni kuuawa katika ghasia na maafisa wa usalama.

Vita hivyo vimeongezeka na kuwaacha takriban watu 3000 wakiwa wameuawa.

Umoja wa Mataifa umegundua makaburi mengi ya halaiki katika eneo hilo.

''Vita hivyo vimewalazimu takriban watu milioni 1.4 kutoroka makwao huku wengine 60,000 wakihamishwa mwezi Juni pekee'', alisema kaimu mkuu wa Unicef nchini DR Congo Tajudeen Oyewale.

Kiongozi huyo wa kitamaduni aliyeuawa alikuwa na wadhfa wa kamuina Nsapu.

Tangu kifo chake makundi tofauti ya wapiganaji wa Kamuina Nsapu yamejitokeza yakipigania malengo tofauti ,lengo lao kuu ikiwa mamalaka.