Mambo kumi yasiyofaa kukupita kuhusu uchaguzi mkuu Kenya 2017

Wapiga kura wakiwa kwenye foleni Haki miliki ya picha AFP/GETTY

Kwa mara nyingine tena, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, wanashindania uongozi wa taifa la Kenya katika uchaguzi wa Agosti baada ya kukabiliana tena Machi 2013.

Rais Kenyatta ni mwana wa rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta naye Bw Odinga mwana wa makamu wa rais wa kwanza Jaramogi Oginga Odinga.

Uchaguzi wenyewe, kuanzia kipindi cha kabla ya kampeni, umeshuhudia mambo ya kipekee. Tumekusanya baadhi hapa:

1) Kuna farasi, punda, mbuni na ngamia

Kinyang'anyiro cha urais kimewavutia wagombea wanane, Uhuru Kenyatta wa Jubilee, Raila Odinga wa Nasa, Cyrus Jirongo wa United Democratic Party (UDP), Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance, Abduba Dida wa Alliance for Real Change (ARC), na wagombea huru Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japheth Kavinga.

Wachanganuzi wanasema ushindani mkali sana ni kati ya Bw Odinga na Bw Kenyatta na hivyo tamko la mbio za farasi wawili limekuwepo, yaani 'Two horse race'.

Wagombea wengine kwa kukerwa na hili nao wamejipa majina yao ya utani. Bw Nyagah, ambaye jina lake maana yake ni mbuni ameamua kujiita 'Mbuni', ndege ambaye ana kasi sana ardhini. Bw Aukot, anayetoka eneo la Turkana, kaskazini magharibi mwa Kenya ambapo kuligunduliwa mafuta, na kuna kisima kifahamikacho kama Ngamia, amejiita Ngamia.

Bw Kaluyu naye amejiita punda, ambaye yuko tayari kubeba mizigo ya wananchi. Viongozi wa upinzani katika mikutano ya hadhara, wamekuwa mara kwa mara wakisema 'Punda Amechoka', kwa maana ya wananchi wamechoshwa na utawala mbaya. Dkt Kaluyu anasema yeye ni punda na raia ni punda wenzake.

2) 'Yaliyo Ndwele Sipite'

Yaliyopita si ndwele, tuyagange yajayo. Wengi wanaifahamu methali hii ya Kiswahili. Lakini mgombea wadhifa wa ugavana katika jimbo la Machakos kwa tiketi ya chama cha Wiper kilicho kwenye muungano wa NASA alipokuwa anawahutubia wanahabari, yamkini ulimi uliteleza. Alisema 'Yaliyo ndwele sipite' badala yake.

Wakenya walianza utani mtandaoni na ghafla kukawa na Shindano la Wavinya.

Wakenya walikuwa wanashindana kutunga methali za Kiswahili kwa kuufuata ulimi wa Wavinya ulioteleza.

Mfano, badala ya Mtoto wa nyoka ni nyoka, Nyoka na mtoto wake ni nyoka. Badala ya Mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani, unapata Mwenda tezi na ngamani marejeo ni omo. Haraka haraka haina baraka inakuwa Baraka baraka haina haraka.

Wengi walifurahia sana utani huo na mchekeshaji MC Njagi akatumia fursa hiyo kutunga wimbo wa utani kwa jina Yaliyo Ndwele Sipite ambao nao pia ulivuma.

Chama cha Jubilee kilitambua ufanisi wa wimbo huo na kumuomba MC Njagi atunge wimbo wa kusifu chama hicho.

Baadaye, MC Njagi pia alitunga wimbo pia wa kumuunga mkono mgombea huyo ambaye ni wa muungano wa Nasa.

3). Safari ya kwenda Canaan

Ukafika Kenya kwa sasa, unaweza kuwasikia baadhi ya wananchi wakizungumzia kuhusu safari ya kwenda 'nchi ya ahadi' - Canaan.

Mbona Wakenya watake kwenda Israel?

Yote yalianza mgombea wa Nasa Raila Odinga alipotangaza kwamba yeye atakuwa kama Joshua anayetajwa kwenye Biblia ambaye aliwavusha wana wa Israeli hadi nchi ya ahadi.

Bw Odinga alitangaza kuwa angekuwa kiongozi wa mpito iwapo atachaguliwa kuongoza Kenya.

„Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya mpito," alisema baada ya kuidhinishwa kuwa mgombea.

Muungano wa Nasa ulianza kuvumisha dhana kwamba ndio muungano unaowapeleka Wakenya nchi ya ahadi Caanan.

Wakenya mtandaoni pia wamekumbatia wazo hilo na kuanza kulifanyia utani mitandao ya kijamii. Kwa kuchukulia safari hiyo kuwa ya kweli, wanajadiliana kuhusu vitu wanavyohitaji kwa safari hiyo, na watu watakaowakuta huko.

Bw Odinga pia hajaachwa nyuma, mfano leo amewasalimia watu na kuwaita 'Watu wa Canaan'.

Haki miliki ya picha TWITTER

4. Mdahalo wa mtu mmoja

Vyombo vya habari viliandaa mdahalo wa wagombea urais kwa mara ya kwanza 2013 na ingawa kulikuwa na wasiwasi kwamba baadhi ya wagombea wangesusia, kila kitu kiliendelea shwari.

Lakini mwaka huu, mambo yalibadilika. Tangu kutolewa kwa tangazo la kuandaliwa kwa mdahalo wa wagombea urais na wagombea wenza, viongozi wa Jubilee na muungano wa upinzani Nasa walitangaza kwamba hawangeshiriki iwapo mabadiliko hayangefanywa. Walidai kwamba hawakushirikishwa wakati wa maandalizi wa mdahalo huo.

Waandalizi waliendelea na mipango yao hata hivyo. Julai 18, mdahalo wa wagombea wenza ulipangwa kufanyika. Sehemu ya kwanza ilishirikisha wagombea sita, na ni mmoja pekee aliyefika - kijana Eliud Muthiora Kariara. Alipewa fursa ya kujieleza na kuulizwa maswali na watangazaji waliokuwa waongoze mdahalo.

Sehemu ya pili ingemshirikisha Naibu Rais William Ruto na makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka lakini hakuna mmoja kati yao aliyefika.

Julai 24, wakati wa mdahalo wa wagombea urais, watatu walifika sehemu ya kwanza, Bw Aukot, Dkt Kaluyu na Prof Wainaina.

Sehemu ya pili iliyosubiriwa kwa hamu, ilikuwa kati ya Bw Odinga na Bw Kenyatta. Bw Odinga alifika lakini Bw Kenyatta alisusia na ikalazimu mdahalo kuendelea na mshiriki mmoja - Bw Odinga aliyeulizwa maswali na watangazaji walioongoza mdahalo.

Image caption Eliud Muthiora Kariara ndiye pekee aliyehudhuria mdahala wa wagombea wenza wa urais

Bw Kenyatta baadaye alisema mdahalo huo ulikuwa wa "kupoteza muda".

5) Wito wa kususia ngono

Tendo la ngono limekuwa likiibuliwa katika siasa nchini Kenya, wengi wakilitazama kama njia inayoweza kuwaongezea nafasi ya kushinda. Mwezi Januari, Mishi Mboko, ambaye ni mwakilishi wa wanawake wa jimbo la Mombasa na anayewania ubunge wa eneo la Likoni, alitoa wito kwa wanawake waliopo katika maeneo yenye wafuasi wengi wa upinzani nchini Kenya kutofanya mapenzi na waume zao ambao hawakuwa wamejisajili kama wapiga kura.

Wakati huo, kila upande ulikuwa ukijaribu kuhamasisha watu kujiandikisha kwa wingi kuwa wapiga kura.

Mwezi Julai, mgombea wa muungano wa upinzani, Nasa, Raila Odinga naye alijitosa kwenye mjadala kuhusu tendo la ndoa na uchaguzi.

Aliwataka wafuasi wake kutoshiriki tendo la ndoa mkesha wa siku ya uchaguzi akifananisha uchaguzi huo na vita akisema kuwa kushiriki ngono kabla ya kwenda vitani ni mkosi mbaya ambao unaweza kusababisha mtu kushindwa.

''Tunaenda vitani na lazima tuhifadhi nguvu zetu kabla ya siku ya vita ambayo ni Agosti 8. Hakuna hata mmoja wetu ambaye anafaa kushiriki ngono kabla ya mkesha wa siku ya uchaguzi," alisema akiwa mjini Homabay eneo la magharibi mwa Kenya.

Haki miliki ya picha AFP

6) Ulevi wakati wa uchaguzi

Tendo la ngono si jambo pekee ambalo wahusika wana wasiwasi kuhusu wakati wa uchaguzi.

Shirika la serikali linalokabiliana na ulevi na dawa za kulevya lina wasiwasi kwamba ulevi huenda ukazuia wengi kupiga kura au kutopiga kura kwa busara.

Shirika hilo, Nacada, mwezi Juni limependekeza baa zifungwe wiki moja kabla ya uchaguzi. Afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Victor Okioma alinukuliwa na runinga ya Citizen akisema Wakenya hawafai kuwa walevi siku ya uchaguzi.

7) Machungwa katika mikutano ya Nasa

Ni kawaida kuwaona watu wakiwa wamejipamba kwa machungwa, au rangi ya chungwa katika mikutano ya muungano wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa).

Asili ya mtindo huu ni chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na mgombea urais Raila Odinga, na ambacho nembo yake ni chungwa.

Chama hicho ni moja ya vyama tanzu vinavyounda muungano huo, kingine kikiwa ni Wiper, chake Kalonzo Musyoka, mgombea mwenza wake Odinga.

Asili ya chama cha ODM na chungwa lenyewe ni mwaka 2005 wakati wa kura ya maoni kuhusu katiba mpya.

Upande uliokuwa ukipinga rasimu ya katiba iliyopendekezwa, ulipewa alama ya chungwa na tume ya uchaguzi nao upande uliounga mkono rasimu hiyo ukapewa alama ya ndizi.

Upande wa Chungwa ulishinda. Mrengo huo uligeuka na kuwa chama.

Upinzani uligawanyika wakati wa uchaguzi wa 2007, ambapo Odinga alikuwa na ODM (alama yake ikiwa chungwa) naye Musyoka ODM Kenya (alama yake ikiwa chungwa nusu). Baada ya uchaguzi wa 2007, Bw Musyoka alibadili chama chake kikawa Wiper Democratic Movement - Kenya (WDM-Kenya), ambacho hujulikana sana kama Wiper.

Bw Musyoka na Bw Odinga waliungana tena chini ya muungano wa Coalition for Reform and Democracy (Cord) mwaka 2013 lakini wakashindwa na Bw Kenyatta.

8. Tano Tena na Tano Fresh

Kauli mbiu ya kampeni ya Bw Kenyatta na Bw Ruto imekuwa 'Tano Tena', yaani Kenyatta na Ruto waongezewe miaka mingine mitano ya kuongoza.

Muungano wa upinzani Nasa kwa upande wake umekuwa ukifanya kampeni yake kwa kauli mbiu ya "Mambo Yabadilika".

Wimbo wa Injili wenye jina hilo wake Hellena Ken umekuwa ukitumiwa kwenye mikutano ya kampeni ya upinzani kusisitiza ujumbe huo. Wimbo wa Amos Barasa na Ridhika Boys Band kwa jina Bindu Bichenjanga kwa maana pia ya mambo kubadilika, pia umekuwa maarufu.

Upinzani, kwa kujibu kauli ya Tano Tena, umekuwa pia ukitumia kauli ya Tano Fresh. Kauli mbiu hiyo inatumiwa pia na wanasiasa wanaopigania kuwaondoa wapinzani wao ambao wamehudumu kwa muhula mmoja, hasa magavana.

Haki miliki ya picha Uhuru Kenyatta / Twitter
Image caption Rais Kenyatta akijibu maswali moja kwa moja kupitia Facebook akiwa ikulu, Nairobi Jumapili

9. Fagia Wote

Kando na kumchagua rais, Wakenya pia watakuwa wakiwachagua wabunge, maseneta, magavana, wawakilishi wa wadi na wawakilishi wa wanawake.

Baadhi ya Wakenya wameonekana kutoridhishwa na utenda kazi wa wanasiasa waliokuwa uongozini tangu 2013.

Baadhi wanaamini wanasiasa waliokuwa uongozini walitumia nyadhifa zao kutetea maslahi yao pekee.

Katika mtandao wa Twitter, kumekuwepo na kampeni inayotumia kitambulisha mada #Fagiawote, kwa maana ya waondoe wote.

Tayari, kuna wanasiasa wengi waliopoteza nafasi zao wakati wa mchujo wa vyama vya siasa.

Haki miliki ya picha Twitter

10. Mbunge anayesubiri kuapishwa

Wengine wakihofia kwamba huenda ufagio wa #FagiaWote huenda ukawanasa, kuna mwanasiasa mmoja ambaye tayari anafurahia ushindi wake.

Kimani Ichung'wa wa chama cha Jubilee hana mtu anayempinga katika eneo bunge lake la Kikuyu, katika jimbo la Kiambu katikati mwa Kenya.

Alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliosifiwa kwa mchango wao ndani na nje ya bunge.

Bw Ichung'wa alikuwa amependekezwa na Jubilee amwakilishwe Naibu Rais William Ruto kwenye mdahalo wa moja kwa moja kwenye runinga uliokuwa unawashirikisha wagombea wenza wa urais. Hakukubaliwa kushiriki, lakini hii ni ishara kwamba anaaminiwa sana na viongozi wa Jubilee.