Utaratibu wa kupiga kura uchaguzi mkuu Kenya 2017

Wapiga kura wakipiga kura

Uchaguzi mkuu nchini Kenya utafanyika tarehe 8 Agosti mwaka 2017 ambapo wapiga kura takriban 19 milioni watamchagua rais, pamoja na wabunge, magavana, maseneta, wawakilishi wa wanawake na madiwani.

Ufuatao ndio utaratibu utakaotumiwa wakati wa kupiga kura.

  • Mpiga kura anafika kituo alichosajiliwa kupiga kura. Mpiga kura anatakiwa kutoa kitambulisho cha kitaifa au pasipoti aliyotumia kujiandikisha.
  • Maafisa wa tume ya uchaguzi watahakiki ikiwa aliyefika amesajiliwa kupiga kura katika kituo hicho, kwa kuweka kidole chake kwenye mtambo wa kuwatambua wapiga kura kwa kutumia alama ya kidole.
  • Mpiga kura atakabidhiwa karatasi sita za kupigia kura - ya rais, mbunge, gavana, seneta, mwakilishi wa wanawake na diwani (mwakilishi wa wadi) - zilizopigwa muhuri.
  • Mpiga kura atasonga hadi eneo la faragha na kumchagua mgombea anayemtaka kwa kuweka alama ndani ya sehemu (kisanduku) iliyotengwa katika karatasi ya kura. Kunja karatasi yako vyema.
  • Tumbukiza karatasi yako ya kura ndani ya sanduku lifaalo kwa kila kura (rais, mbunge na kadhalika).
  • Kidole chako kitapakwa rangi isiyofutika kwa urahisi kuzuia watu waliopiga kura kurudia kupiga kura tena.
  • Ondoka kutoka kituo cha kupiga kura.

Jinsi ya kumchagua mgombea kwenye karatasi ya kura

Kuna sababu nyingi ambazo husababisha kura kuharibika na hivyo kutohesabiwa.

Kuu zaidi huwa ni mpiga kura kuweka alama kwa njia isiyofaa wakati wa kuchagua mgombea au chama anachokitaka.

IEBC inasema mpiga kura anatakuwa kuweka "alama kwenye nafasi iliyotengwa kwa jina la chama/mgombeaji au picha ya chama ungependa kuchagua."

Mpiga kura anafaa "kuweka alama kwa mgombeaji mmoja tu." Hufai kuweka alama yeyote nyingine kwenye karatasi ya kura. Alama unayoweka inaweza kuwa alama ya ndio (✓), mkasi (✕), au hata alama ya kidole. Hata hivyo, huruhusiwi kuandika jina lako au kuweka sahihi yako kama alama ya kumchagua mgombea unayemtaka. Iwapo utafanya makosa bila kukusudia wakati wa kuweka alama yako kwenye karatasi ya kura na utambue hilo kabla ya kutumbukiza karatasi yako kwenye sanduku, unaweza kupewa karatasi nyingine ya kura. Unaweza kupewa karatasi mpya ya kura mara mbili pekee.

Baada ya kumaliza kuweka alama, unafaa kuikunja karatasi katikati kutoka kushoto kwenda kulia ili kuweka siri uliyemchagua halafu utumbukize karatasi hiyo kwenye sanduku lifaalo.

Tume ya uchaguzi imepiga marufuku kurandaranda katika kituo baada ya kupiga kura. Vile vile, ni hatia kupiga picha katika kituo cha kupiga kura au kupiga picha karatasi za kura.