Wanaharakati waandamana kushutumu mauaji ya meneja wa tume ya uchaguzi Kenya

Waandamanaji
Image caption Waandamanaji wamebeba mabango kuunga mkono tume ya uchaguzi

Watetezi wa haki za kibinadamu wameandamana katika uwanja wa Uhuru Park, kushutumu kuuawa kwa afisa mmoja mkuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya Christopher Msando.

Bw Msando alitoweka Ijumaa na mwili wake ukapatikana ukiwa umetumwa viungani mwa jiji la Nairobi Jumamosi asubuhi.

Mwili wake ulitambuliwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City Jumatatu.

George Kegoro kutoka shirika lisilo la kiserikali la Tume ya Haki za Kibinadamu Kenya (KHRC) amesema wana wasiwasi sana kwamba mauaji ya Bw Msando yatazua mtafaruku uchaguzi mkuu unapokaribia.

Waandamanaji walikuwa wamebeba mabango wakihimiza umuhimu wa tume ya uchaguzi IEBC, kutoingiliwa. Wamesema sababu pekee ya kumuua afisa huyo aliyekuwa akisimamia mfumo wa teknolojia wa uchaguzi katika tume hiyo ni kuingilia uchaguzi wenyewe na kwamba hilo huenda likachochea ghasia.

Waandamanaji hao walikuwa wamepanga kuandamana hadi afisi za mkuu wa polisi Joseph Boinnet na makao makuu ya IEBC.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, kupitia taarifa baada ya kutambuliwa kwa mwili wa Bw Msando, alikuwa ametoa wito kwa polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo chake.

"Tume itamteua wakili huru wa kushirikiana na Mkuu wa Polisi katika uchunguzi. Tunataka haki kwa Chris, Haki kwa IEBC na Haki kwa Taifa."

Bw Wabukati alikuwa pia amemuomba mkuu wa polisi kuimarisha ulinzi kwa makamishna na maafisa wakuu wa tume hiyo.

Mada zinazohusiana