Msemaji wa jeshi aliyedaiwa kutoweka ajitokeza Kenya

Kanali Owuoth aliandamana na Waziri Omamo katika kikao na wanahabari
Image caption Kanali Owuoth (kulia) aliandamana na Waziri Omamo katika kikao na wanahabari

Wizara ya ulinzi nchini Kenya imeshutumu taarifa zilizokuwa zimeenezwa kwamba msemaji wa jeshi la Kenya Kanali Joseph Owuoth alikuwa ametoweka.

Waziri Raychelle Omamo, akihutubia wanahabari, amesema taarifa kama hizo zinatishia usalama na kuzua wasiwasi miongoni mwa maafisa wa jeshi na familia zao.

"Kanali J. M. Owuoth hajatoweka na yuko nasi hapa, akiwa hai na mzima wa afya," alisema Bi Omamo.

"Tunawataka wanasiasa kukaa kutoiingiza wizara katika siasa zao."

Kanali huyo alikuwa ameandamana na waziri kwenye kikao hicho.

Kanali Owuoth aligonga vichwa vya habari baada ya kuthibitisha kwamba nyaraka zilizokuwa zimetumiwa na muungano wa upinzani nchini humo Nasa kudai kwamba serikali inapanga kutumia jeshi kutekeleza 'mapinduzi' ili kuendelea kusalia madarakani zilikuwa halisi.

Msemaji huyo hata hivyo alisema nyaraka hizo zilinukuliwa na kufasiriwa visivyo.

Bi Omamo, kwenye kikao hicho, alisema baada ya uchunguzi, imebainika kwamba nyaraka hizo zilizotumiwa na muungano wa Nasa zilikuwa ghushi.

Taarifa za kudaiwa kutoweka kwa Kanali Owuoth zilikuwa zimezua wasiwasi mkubwa kwani zilijiri siku moja baada ya mwili wa meneja wa teknolojia katika Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC) Chris Msando, aliyetoweka Ijumaa usiku, kupatikana katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City jijini Nairobi pamoja na mwili wa mwanamke mwingine.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliambia wanahabari kwamba hakukuwa na shaka kwamba Bw Msando aliteswa kabla ya kuuawa na kuwataka polisi wafanye uchunguzi wa kina kufumbua kitendawili kuhusu kuuawa kwake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii