30 wafariki katika mlipuko mskitini Afghanistan

mskiti Afghanistan Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mlipuko umesababisha uharibifu katika mskiti huko Herat

Milipuko na risasi zilizofyetuliwa katika mji uliopo Afghanistan magharibi - Herat imesababisha vifo vya watu takriban 30 na kusababisha wengine wengi kujeruhiwa.

Msemaji wa polisi katika eneo hilo amesema shambulio hilo limetekelezwa na mlipuaji wa kujitoa muhanga.

Hakuna kundi linalodai kuhusika.

Shambulio dhidi ya Mskiti wa Jawadia limetokea saa mbili usiku wakati mamia ya waumini walipokuwa wanaswali swala ya jioni.

Mskiti huo upo katika eneo la mji wa Herat ulio na idadi kubwa ya wasilamu wa madhehebu ya Shia.

Afisa wa serikali ameiambia BBC kwamba mlipuaji wa kujitoa muhanga alifyetua risasi ndani ya mskiti kabla ya kujilipua.

Herat, mji uliopo karibu na mpaka na Iran, unatazamwa kuwa mojawapo ya miji ya amani Afghanistan.

Katika mwaka uliopita, kundi la Islamic State limelenga maeneo ya Shia katika sehemu nyingi nchini.

Siku ya Jumatatu kundi hilo limekiri kuhusika na shambulio la kujitoa muhanga dhidi ya ubalozi wa Iraq katika mji mkuu Kabul.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii