Rais wa Brazil Temer aponea kura ya rushwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Muhula wa Rais Temer unamalizika Desemba 2018

Bunge la Brazil limepiga kura kutomshtaki rais Michel Temer kwa tuhuma za rushwa.

Wabunge wa upinzani katika bunge la wawakilishi walishindwa kupata uwingi wa thuluthi mbili unaohitajika kuwasilisha kesi katika mahakama ya juu zaidi.

Rais Temer amekaribisha kura hiyo na kuitaja kuwa "ya wazi na isiyopingika".

Kiongozi huyo ametuhumiwa kupokea $12milioni kama rushwa kutoka kwa mkuu wa kampuni kubwa ya nyama JBS. Amekana tuhuma hizo.

Katika bunge la viti 513, 263 walipinga hoja hiyo huku 227 wakiunga mkono hoja hiyo, kiwango kilichosathili kupitisha hoja hiyo ni kura 342.

Ameahidi kukamilisha muhula wake madarakani unaomalizika Desemba 2018.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wabunge walibeba vikaragosi bungeni vya rais wa zamani Lula, hatua iliyowakasirisha wafuasi wa upinzani.

Ghasia zilitatiza vikao vya bunge huku wabunge wakijibizana.

Wabunge walisukumana , na kurusha pesa bandia kwa wapinzani wao.

Wafuasi wa rais Temer wamelalamika kuwa kutimuliwa kwake kutasababisha ghasia na kuathiri uchumi ulio mbaya wa Brazil.

Temer aliingia uongozini mwaka jana kufuatia kura ya kutokuwana imani dhidi ya kiongozi aliyemtangulia, Dilma Rousseff.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii