Mfahamu rais 'wa kidijitali' Uhuru Kenyatta

Uhuru Kenyatta

Chanzo cha picha, AFP

Rais Uhuru Muigai Kenyatta aliibuka kuwa rais wa umri mdogo zaidi kuwahi kuongoza Kenya aliposhinda uchaguzi mkuu wa Machi mwaka 2013 akiwa na mgombea mwenza wake William Samoei Ruto.

Mwaka 2017 wakati wa uchaguzi mkuu, hali ilikuwa tofauti sana lakini walifanikiwa kushinda urais kwa kupata kura 8,203,290 ambayo ni sawa na asilimia 54.27 ya kura zilizopigwa wakati wa uchaguzi wa tarehe 8 Agosti.

Lakini Mahakama ya Juu ilifutilia mbali uchaguzi huo na kusema ulijaa kasoro nyingi. Mahakama hiyo ikiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga iliagiza uchaguzi mpya ufanyike.

Tume ya taifa ya uchaguzi IEBC iliandaa uchaguzi huo 26 Oktoba lakini kiongozi wa upinzani Raila Odinga akasusia.

Kwa mara ya pili Kenyatta alitangazwa mshindi tena akiwa na kura 7.5 milioni sawa na asilimia 98, ambapo waliojitokeza walikuwa asilimia 39 pekee.

Walipokuwa wanawania mwaka 2013, Kenyatta na Ruto walikuwa wanakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi, jambo ambalo lilichangia pia kuwaleta wawili hao pamoja kisiasa, na kuunganisha jamii zao.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007, Bw Kenyatta na Bw Ruto walikuwa katika pande pinzani, Kenyatta akiunga mkono Rais Mwai Kibaki aliyekuwa anapigania kuchaguliwa tena naye Bw Ruto akimuunga mkono Raila Odinga wa chama cha ODM.

Wawili hao walijipigia debe kwa wananchi kama viongozi wa kisasa, vijana wa kuleta mabadiliko - kwa kifupi viongozi wa dijitali. Waliwabatiza wapinzani wao kuwa wazee waliosimamia mambo ya zamani - analogu.

Lakini wakati mwaka 2017, mambo yalibadilika. Rais Kenyatta alitetea kuchaguliwa tena kwa msingi wa aliyoamini alikuwa ametimiza na serikali yake kwa miaka minne na miezi kadha ambayo alikuwa uongozini.

Chini ya uongozi wake, mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kati ya Mombasa na Nairobi ulikamilishwa na wananchi sasa wanaweza kusafiri kwa saa nne safari ambayo awali ilikuwa ikichukua saa zaidi ya nane.

Kwa kujaribu kutimiza sifa zake kama kiongozi wa kidijitali, serikali yake ilijaribu kutimzia ahadi ya kuwapa wanafunzi wa shule za msingi vipakatalishi.

Mradi huo ulikuwa na changamoto awali - ahadi ilikuwa kuwapa watoto wa darasa la kwanza vipakatalishi, na baadaye kila watoto wanaojiunga na shule ya msingi kila mwaka kuhakikisha mwishowe wanafunzi wote shule za msingi wana vipakatalishi.

Mpango huo ulibadilishwa na badala yake wanafunzi wamekuwa wakipewa tabiti.

Serikali ya Bw Kenyatta pia ilizindua vituo maalum vya kutoa huduma za serikali kwa jumla sehemu moja - Vituo vya Huduma. Kupitia vituo hivyo, Wakenya wanaweza kupata na kulipia huduma kama vile ulipaji kodi, vitambulisho, leseni za udereva, huduma ya bima ya taifa ya hospitali na kadhalika.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Bw Kenyatta na Bw Ruto walijipigia debe 2013 kama viongozi wa kizazi kipya

Serikali yake pia ilianzisha tovuti ya kutumiwa na wananchi kufuatilia utekelezaji wa miradi iliyoahidiwa na serikali. Aidha, kulikuwa na tovuti ya kupiga ripoti mara moja kuhusu visa vya ulaji rushwa moja kwa moja hadi kwa rais.

Wakosoaji wake hata hivyo wamesema mingi ya miradi hiyo ni ya kujipendekeza kwa wananchi lakini haijaimarisha uwazi na pia haijasaidia kupiga vita ulaji rushwa.

Bw Kenyatta ana wafuasi wengi sana Facebook na kwenye Twitter na huwa mara kwa mara anafuata mitindo inayovuma mtandaoni.

Mfano aliwahi kucheza dansi ya dab ilipokuwa inavuma.

Wakati wa kampeni, alifanya vikao viwili moja kwa moja kwenye Facebook kupokea na kujibu maswali ya wananchi.

Rais Kenyatta alizaliwa Oktoba 26 mwaka 1961, akiwa mwana wa rais wa kwanza wa Mzee Jomo Kenyatta na mke wake wa nne Mama Ngina Kenyatta.

Alilelewa katika maisha ya utajiri na kusomea shule za kifahari zikiwemo shule ya St Mary's, Nairobi. Alipomaliza masomo ya upili, alifanya kazi kwa muda kama karani wa benki ya Kenya Commercial Bank (KCB) tawi la Kipande House, Nairobi kabla ya kuelekea Chuo cha Amherst katika jimbo la Massachusetts nchini Marekani ambapo akasomea na kuhitimu na shahada ya sayansi ya siasa.

Baada ya kurejea Kenya, alijishughulisha na biashara hasa kilimo cha mboga na matunda. Alianza kuchangia katika usimamizi wa biashara za familia.

Kenyatta alianza kujiingiza katika siasa miaka ya 1990 na mwaka 1997 alikuwa mwenyekiti wa tawi la chama tawala cha wakati huo Kenya African National Union (KANU) katika eneo lake la Gatundu.

Aliwania ubunge katika eneo bunge la Gatundu Kusini uchaguzi mkuu wa mwaka 1997 kupitia chama cha KANU lakini akashindwa na Moses Muihia wa chama cha Democratic Party kilichokuwa na Mwai Kibaki.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais mstaafu Moi (kulia) alimkuza Uhuru Kenyatta kisiasa

Wengi walitarajia kuwa angeshinda lakini baada ya kushindwa, Uhuru alighadhabika sana na hata kuahidi kuasi siasa.

Wengi waliona hatua ya Moi kama kumtayarisha Uhuru kwa mambo makubwa katika siku za baadaye.

Mara moja akarejea katika biashara za familia yake ambazo zinajumuisha hoteli tano mashuhuri, kampuni za vifaa vya ndege na kilimo cha biashara. Lakini hakujua kuwa Moi bado alikuwa na mpango naye kutaka kumpeleka katika ngazi za juu.

Kwa miaka miwili, hakusikika sana hadi pale mwaka 1999 alipoteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Kenya (KTB) na Rais Daniel Moi.

Mwaka uliofuata, Bw Moi alimteua kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kuratibu Juhudi za Kukabiliana na Majanga.

Mwaka 2001, mwezi Oktoba, aliteuliwa na Moi kuwa mbunge maalum Kenyatta's political profile rose considerably in October 2001 baada ya mbunge maalum Mark Too kushawishiwa ang'atuke.

Rais Moi kisha alimteua na kuwa waziri wa serikali za mitaa mwezi mmoja baadaye.

Mwaka 2002, alichaguliwa kuwa mmoja wa wenyekiti wanne wa chama cha Kanu, na baadaye akataidhinishwa kwua mgombea urais wa chama hicho.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 27 Desemba, 2002, Kenyatta alishindwa na mgombea wa upinzani Mwai Kibaki aliyepata asilimia 62 ya kura, Bw Kenyatta naye akapata asilimia 31. Wakati huo, Kenyatta alipuuziliwa mbali kama 'mradi wa Moi', na wengi hawakutarajia kwamba nyota yake kisiasa ingeendelea kung'aa.

Kwa muda, alitaka kuonyesha watu kuwa yeye anaweza kujitegemea mwenyewe wala sio kibaraka cha Moi kama wengi walivyokuwa wanasema.

Kiongozi wa upinzani na wa chama

Katika bunge jipya alikuwa kiongozi wa upinzani lakini alipata pia upinzani ndani ya chama hasa kutoka kwa kigogo wa chama cha KANU Nicholas Biwott pamoja na wanasiasa kutoka Bonde la Ufa.

Januari 2005 alimshinda Biwott walipogombea uwenyekiti wa chama hicho na hapo Biwott akondoka chamani na kuunda chama chake cha New Kanu.

Katika kura maalumu ya wananchi kuhusu katiba mpya Uhuru aliungana na viongozi wengine katika kambi ya Chungwa wakiwemo Bw Raila Odinga na Kalonzo Musyoka na kufanikiwa kuushinda upande wa Serikali.

Viongozi walioipinga rasimu ya katiba iliyokuwa imependekezwa wakati huo waliungana na kuunda chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

Mipango yake ya kushiriki katika harakati za ODM zilipingwa vikali ndani ya chama kwa sababu viongozi wengine wa KANU pamoja na rais mstaafu Moi waliogopa kuwa chama hicho cha uhuru Kenya kingeangamia.

Novemba 2006 Biwott alirudia jaribio la kumpindua Uhuru kwa kuitisha mkutano wa Kanu mjini Mombasa bila idhini ya mwenyekiti wala kamati ya chama.

Hapa alichaguliwa kuwa mweyekiti mpya. Kwa msaada wa serikali Biwott alifaulu kuandikisha kamati yake kama uongozi rasmi hivyo kumwondoa Uhuru katika nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni.

Uhuru alipinga na Mahakama Kuu ikabatilisha kura ya Mombasa tarehe 29 Desemba 2006, na baadaye uamuzi huo ukathibitishwa Juni 2007, na kuamua kwamba hakukuwa na ushahidi wowote kuthibitisha madai ya Bw Biwott na wenzake kwamba Bw Kenyatta alikuwa amehamia chama kingine.

Kuhamia upande wa Kibaki 2007

Juni 2007 Uhuru alionyesha wazi ya kwamba alitaka kuacha ushirikiano wa ODM kwa kutopeleka jina lake kati ya wagombea wa urais upande wa ODM.

Badala yake alieleza ya kuwa atampigania rais Kibaki achaguliwe tena. Alisema hana nia ya kugombea urais ikiwa hana uhakika kuwa atashinda.

Kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata, Kibaki alitawazwa kama rais licha ya utata huo. Kibaki naye alimteua Uhuru kama waziri wa serikali za mitaa na baada ya mapatano kati ya Kibaki na Odinga, Uhuru aliteuliwa kama naibu waziri mkuu ikiwa ni sehemu ya mpango wa kugawana mamlaka.

Aliondolewa kuwa waziri wa serikali za mitaa na kuteuliwa waziri wa fedha mwaka 2009.

Kuchaguliwa rais mwaka 2013

Safari yake ya kisiasa ilichukua mwelekeo mpya Desemba 15, 2010 alipotajwa na mahakama ya ICC kama mmoja wa wahusika wakuu katika ghasia za baada ya uchaguzi. Alituhumiwa kupanga na kufadhili ghasia katika maeneo ya Naivasha na Nakuru.

Uchaguzi wa mwaka 2013 ulipokaribia, alijitosa kwenye kinyang'anyiro cha urais kupitia chama cha The National Alliance (TNA) ambapo alishirikiana na William Ruto wa chama cha United Republican Party (URP).

Alishinda urais kwa kupata asilimia 50.7 dhidi ya Raila Odinga wa chama cha ODM aliyepata asilimia 43.4.

Alihudhuria vikao katika mahakama ya ICC Novemba mwaka 2014 lakini tarehe 13 Machi, 2015 mashtaka dhidi yake yaliondolewa.

Kutengwa na jamii ya kimataifa

Kutokana na mashtaka yaliyomkabili yeye na Bw Ruto mahakama ya ICC wakati wa uchaguzi wa mwaka 2013, wapinzani wao walionya kuwa Kenya ingetengwa na jamii ya kimataifa.

Serikali za Marekani na Uingereza ziliwatahadharisha Wakenya kwamba hali haingesalia kuwa ya kawaida iwapo Bw Kenyatta na Bw Ruto wangechaguliwa.

Bw Kenyatta alirejelea hilo majuzi wakati wa uzinduzi wa manifesto ya chama chake cha sasa cha Jubilee.

"Walitwambia kwamba ulimwengu ungetutenga, lakini sasa hakuna taifa linalokataa kukutana na rais wa jamhuri ya Kenya," alisema.

Wakati wa uongozi wa Kenyatta, Kenya imekuwa mwenyeji wa makongamano na mikutano mingi ya kimataifa. Kadhalika, Kenya imewapokea watu mashuhuri akiwemo aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama na kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama ni miongoni mwa viongozi waliozuru Kenya wakati wa utawala wa Kenyatta

Bw Kenyatta pia alifanikiwa kupata uungwaji mkono wa nchi za Afrika kutishia kujiondoa kutoka kwa ICC iwapo mahakama hiyo haingefutilia mbali kesi dhidi yake na Bw Ruto.

Kenya imesalia kuwa mshirika mkuu wa Marekani na Uingereza na nchi nyingine za Magharibi, hasa katika kukabiliana na wanamgambo wa al-Shabab nchini Somalia.

Bw Kenyatta huwa sana hana kipaji cha kutoa hotuba ndefu kwa umma lakini sauti yake huwa na nguvu na ushawishi, hasa anapotetea jambo au kujitetea.

Mamake alihakikisha kwamba licha ya kulelewa katika maisha ya kifahari, anafahamu vyema lugha ya mama.

Huwa anaitumia vyema kuwavutia watu kutoka kwa jamii yake ya Wakikuyu.

Wenyewe hupenda kumuita kwa utani "Kamwana", maana yake "kijana".

Maelezo ya picha,

Reli ya kisasa ya SGR nchini Kenya iliyozinduliwa ilikuwa ni matokeo ya maafikiano kati ya Serikali ya Kenya na China ambapo China ilifadhili asilimia 80 na Kenya ikafadhili asilimia 20 iliyobaki.

Utajiri na vyombo vya habari

Bw Kenyatta ameorodheshwa na jarida la Forbes kama mtu wa 26 kwa utajiri Afrika ambapo utajiri wake unakadiriwa kuwa takriban $500m (£320m).

Ana usemi pia katika umiliki wa vyombo vya habari - familia ya Kenya humiliki kampuni ya Mediamax inayomiliki runinga ya K24, gazeti la The People na vituo kadha vya redio.

Familia ya Kenyatta pia imewekeza sana katika utalii, benki, ujenzi, maziwa na bima.

Aidha, wanamiliki mashamba makubwa Bonge la Ufa, maeneo ya kati na pwani.

Suala la ardhi limekuwa likijitokeza mara kwa mara kuhusu uongozi wa Kenyatta kila aendako.

Suala la umiliki wa ardhi limekuwa chanzo cha mapigano ya kikabila ya mara kwa mara Bonde la Ufa. Miaka minne aliyokuwa uongozini, serikali yake imejitahidi kutoa hati miliki za ardhi kwa wakazi wa maeneo mengi, na hasa pwani.

Kukosolewa muhula wa kwanza uongozini

Wakosoaji wa Bw Kenyatta wanasema wakati wa uongozi wake ameminya uhuru wa kujieleza na uhuru wa wanahabari.

Mwaka 2016, mwanahabari wa gazeti la kibinafsi linalosomwa zaidi Kenya Daily Nation, alifutwa kazi kwa kuandika tahariri ambayo ilikosoa serikali.

Godfrey Mwapembwa, mchoraji vibonzo maarufu kwa jina Gado, naye alidaiwa kufutwa kwa kuchora vibonzo vilivyoikosoa serikali mra akwa mara.

Kiuchumi, swali kuu ni: Wakenya wako heri sasa kuliko walivyokuwa mwaka 2013?

Uchumi wa Kenya umekuwa ukikua kwa kiwango cha wastani cha asilimia 5 kila mwaka tangu aingie uongozini, lakini baadhi ya Wakenya wanasema hawajahisi manufaa ya ukuaji huo.

Maelezo ya picha,

Unga wa mahindi uliadimika na kupanda bei hadi ikalazimu serikali iingilie kati

Kwa miezi mitatu hivi, kumekuwa na uhaba mkubwa wa unga wa mahindi na gharama ya bidhaa nyingi muhimu imepanda.

Serikali yake pia imetuhumiwa kuchukua mikopo kwa wingi, baadhi wakikadiria kwamba serikali hiyo imepitisha viwango vya ukopaji vya serikali zote za awali tangu uhuru. Deni la sasa la taifa hilo ni $26bn (£20bn).

Bw Kenyatta, hata hivyo amesema kuwa uwekezaji wa pesa hizo katika miradi ya miundo mbinu, mfano reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi iliyogharimu $3.2bn (£2.5bn), itasisimua ukuaji wa uchumi.

Rais Kenyatta aliahidi kuangamiza ufisadi lakini mwanaharakati John Githongo anasema serikali ya Kenyatta imekuwa ndiyo "fisadi zaidi katika historia ya Kenya".

Katika ripoti ya maoni kuhusu viwango vya ufisadi ya 2016 Transparency International Kenya iliorodheshwa nambari 145 kati ya nchi 176.

Bw Kenyatta amekuwa akisema juhudi zake za kukabiliana na ufisadi zimehujumiwa na mahakama na mamlaka ya kupambana na rushwa.

Mwaka 2015, Kenyatta aliwasimamisha kazi na kisha akawafuta mawaziri watano na maafisa wengine wa ngazi ya juu serikali waliotuhumiwa kujihusisha katika ufisadi. Waziri mwingine alijiuzulu kutoka na shinikizo kutoka kwa umma.