Ekuru Aukot: ‘Daktari wa Katiba’ anayetaka kuwa rais Kenya

Dkt Ekuru Aukot

Baadhi humfahamu kama Daktari wa Katiba kutokana na mchango wake katika kupatikana kwa Katiba Mpya nchini Kenya ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 2010.

Dkt Ekuru Aukot, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya katiba, alikuwa mkurugenzi na afisa mkuu mtendaji wa wa Kamati ya Wataalamu iliyohusika katika kuandika rasimu ya katiba hiyo.

Sasa, anataka kuwa rais wa taifa la Kenya kutokana na kile anachosema ni kutoheshimiwa na kuhujumiwa kwa Katiba aliyosaidia kuwepo kwake.

Dkt Aukot alizaliwa miaka 45 iliyopita katika eneo la Kapedo, katika kaunti ya Turkana kaskazini magharibi mwa Kenya.

Babake, Mzee Aukot Tarkus, alikuwa na wake wanne na watoto 27.

Kutokana na migogoro iliyokumba eneo hilo, Aukot anasema alisomea elimu ya msingi katika shule sita tofauti.

Alisomea shahada ya uanasheria Chuo Kikuu cha Nairobi na kufuzu 1997 na mwaka 1999 akahitimu kama mwanasheria katika Chuo cha Wanasheria Kenya.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Warwick nchini Uingereza na kufuzu na shahada ya uzamili (Sheria na Maendeleo) na uzamifu (Sheria ya Kimataifa kuhusu Wakimbizi) katika uanasheria.

Alifundisha masuala ya Sheria ya Katiba na Utawala katika chuo kikuu cha Warwick kati ya 2005-2005 na baadaye akafundisha katika Chuo cha Uanasheria Kenya kati ya mwaka 2006 na mwaka 2009.

Alianzisha chama cha Thirdway Alliance katika juhudi za kutoa uongozi mbadala na uongozi wa mageuzi kwa Wakenya.

Anaamini Wakenya hawawezi kuwategemea tena viongozi ambao wamekuwa madarakani kufikia sasa kumaliza ufisadi na ukabila.

Mwaka 2011, Dkt Aukot aliteuliwa kuhudumu kama mwenyekiti wa jopo la uteuzi lililohusika kuwateua makamishna wa kwanza wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kutambuliwa kimataifa

Mafanikio yake katika kupatikana kwa katiba mpya Kenya yalimfanya kupata kazi karibu sawa na hiyo mataifa mbalimbali barani Afrika.

Alihudumu kama mshauri mkuu wa masuala ya kiufundi wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo (UNDP) katika Kamati ya Marekebisho ya Katiba nchini Liberia.

Huwezi kusikiliza tena
Kwa nini Ekuru Aukot anataka kuwa rais Kenya?

Mwaka 2016, nchini Lesotho alisaidia kuchora ramani ya shughuli ya marekebisho ya katiba nchini humo.

Ametoa mihadhara na kutoa ushauri kuhusu marekebisho ya katiba katika nchi nyingine kama vile Misri, Tunisia, Sudan Kusini, Zimbabwe, Zambia, Ukraine, Ujerumani, mjini the Hague na vyuo vikuu kadha Marekani.

Dkt Aukot ni miongoni mwa wanasiasa wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza ujumbe wao.

Huandika ujumbe na kuchangia sana mijadala kwenye Twitter ambako ana wafuasi 79,000 kufikia sasa.

'Mbio za ngamia na farasi'

Dkt Aukot ana watoto wawili na ndiye mwanzilishi na rais wa Wakfu wa Ekuru Aukot, ambao huwasaidia watoto kutoka kwa jamii za wafugaji kupata elimu.

Baadhi wameeleza kinyang'anyiro cha urais mwaka huu kuwa tena 'mbio za farasi wawili' kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Dkt Aukot hata hivyo anaamini anaweza kushinda uchaguzi. Anajitazama kama ngamia, ambaye ana ukakamavu na nguvu za kuendelea na safari hata nyakati za shida na pia mwendo wake ni wa kasi na wa uhakika.

"Kenya inahitaji mtu wa mbio za masafa marefu," anasema Aukot.

Jimbo la Turkana pia ndiko kulikogunduliwa mafuta nchini Kenya na kuna kisima maarufu kwa jina Ngamia.

Mada zinazohusiana