Cyrus Jirongo: Mwanasiasa mwanabiashara anayetaka kuongoza Kenya

Jirongo Haki miliki ya picha Team Jirongo/Facebook

Uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini Kenya ulipokaribia mwaka 1992, kundi la vijana lilijitokeza kujaribu kumsaidia Rais wa wakati huo Daniel arap Moi kukabiliana na wimbi la upinzani.

Kundi hilo lilikuwa na jina la Youth for Kanu '92 (YK '92).

Kiongozi wa kundi hili alikuwa Shakhalaga Khwa Jirongo ambaye hufahamika sana kama Cyrus Jirongo.

Bw Jirongo alizaliwa 21 Machi, 1961 na alisomea shule ya upili ya Mang'u kati ya 1978 na 1981 na kisha akafuzu kutoka Chuo Kikuu cha Egerton mwaka 1986.

Mwaka 1991, alikuwa mwenyekiti wa klabu kongwe ya soka nchini Kenya AFC Leopards.

Mwaka 1997, aliwania ubunge katika eneo la Lugari, magharibi mwa Kenya ana akashinda kupitia chama cha Kanu. Miaka miwili baadaye hata hivyo, alianza kutofautiana na viongozi wa chama hicho na akaanza kuhusishwa na chama cha United Democratic Movement ambacho kilipigania mageuzi ya katiba.

Aliteuliwa waziri wa maendeleo ya nyanjani mwaka 2002 miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu. Hata hivyo alishindwa uchaguzini.

Aliunda chama kipya cha kisiasa kwa jina Kenya African Democratic Development Union (KADDU) mwaka 2006 na akafanikiwa kuwania kiti cha eneo bunge la Lugari uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Matokeo ya uchaguzi huo yalikumbwa na utata na kukaundwa serikali ya umoja wa taifa. Chama chake, ambacho alikuwa mbunge wake pekee bungeni, hakikushirikishwa.

Septemba 2012, alikuwa ametangaza nia ya kuwania urais kupitia chama cha Federal Party of Kenya (FPK).

Haki miliki ya picha Team Jirongo/Facebook
Image caption Jirongo alikuwa katika chama cha FPK mwaka 2012

Alibadilisha nia yake mwishoni mwa mwaka huo na badala yake akaamua kumuunga mkono mgombea wa Cord Raila Odinga na kuwania useneta katika kaunti ya Kakamega.

Alishindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Machi 2013 na mgombea wa Ford Kenya Dkt Bonni Khalwale.

Jirongo alizindua azma yake ya kuwania tena urais Januari mwaka huu kupitia chama cha United Democratic Party.

Mwezi uliopita, mahakama ilitupilia mbali ombi lake la kutaka uamuzi wa Benki Kuu ya Kenya wa kuweka kampuni yake chini ya mrasimu kutokana na mkopo wa Sh495 milioni ambao kampuni moja yake ilidaiwa na benki iliyofilisika ya Dubai Bank.

Kufuatia hatua hiyo ya benki, wapiga mnada wa Valley Auctioneers waliuza kupitia mnada ardhi ya eka 103 iliyomilikiwa na kampuni yake ya Kuza Farms & Allied Limited karibu na mji wa Eldoret, kaskazini magharibi mwa Kenya kwa mujibu wa gazeti la kibinafsi la Daily Nation.

Bw Jirongo ni miongoni mwa wagombea ambao hawajakuwa wakionekana sana kwenye vyombo vya habari.

Aidha, alikuwa miongoni mwa waliosusia mdahalo ulioandaliwa na vyombo vya habari mwishoni mwa Julai akiwa pamoja na Joseph Nyagah, Abdouba Dida na Rais Uhuru Kenyatta.

Mada zinazohusiana