Kwa nini maradhi ya marais huwa siri?

Rais Mugabe ni mmoja kati ya viongozi walio katika nafasi ya Urais kwa muda mrefu zaidi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Mugabe ni mmoja kati ya viongozi walio katika nafasi ya Urais kwa muda mrefu zaidi

Afya ya marais hasa kutoka bara la Afrika mara nyingi imekuwa ikigubikwa na usiri wa hali ya juu. Ni mara chache sana, rais anapoondoka kwenda nje ya nchi kwa matibabu husema hadharani.

Mara nyingi, safari hizo hufanywa kimya kimya au mara nyingine, huambatanishwa na safari rasmi ili kupoteza malengo.

Kumekuwa na hiyo hofu kwamba, iwapo itafahamika kwamba rais au kiongozi yoyote wa nchi anaugua au anasumbuliwa na aina fulani ya maradhi, basi pengine mahasimu wake wa kisiasa wanaweza kuutumia mwanya huo, au kunaweza kuwa na hofu kwamba rais hataweza kutekeleza majukumu yake ya kila siku kutokana na kuumwa.

Image caption Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na mkewe

Pengine ndio hofu hiyo ambayo imewalazimu marais wawili kutoka nchi za Afrika ambao wamekuwa madarakani kwa muda mrefu pengine kuliko marais wa nchi nyengine za bara hili, hivi karibuni wakijigamba hadharini kuhusu afya zao.

Kwanza ameanza rais Robert Mugabe wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 93, akiwa katika mkutano wa hadhara katika mji wa Chinhoyi, alisema, "Kuna wanaosema kuwa rais anaondoka. Mimi siondoki. Wengine wanasema rais anakufa. Mimi sifi."

Matamshi hayo ya rais Mugabe yalikuwa ni majibu kwa mke wake Grace ambae amekuwa akimshawishi kutaja mrithi wake.

Hata hivyo, wakati akisema hayo, Mugabe amekuwa akisafiri mara kwa mara kwenda nchini Singapore kwa ajili ya matibabu.

Safari yake ya hivi karibuni ni ile ya mwanzoni mwa mwezi wa saba mwaka huu. Lakini licha ya majigambo hayo, Mugabe, mara kwa mara amekuwa akitembea kwa kujivuta huku akitumia muda wake mwingi kusinzia katika mikutano.

Haijachukua muda mrefu baada ya rais Mugabe kujisifu hadharani kuhusu afya yake.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Akiwa katika wilaya ya Budaka, rais Yoweri Museveni amewaambia waganda waliojitokeza katika viwanja vya Budaka Ssaza kuwa hajawahi kuugua katika kipindi cha miaka 31 aliyokuwa madarakani.

Rais Museveni, ametaja mafanikio yake kuwa yanatokana na kula vizuri, kunywa maji safi, na kusema kuwa baadhi ya maradhi yanaepukika.

"Je, mshawahi kusikia kuwa Museveni anaumwa na amelazwa hospitalini katika kipindi cha miaka 31 iliyopita," alidhihaki Museveni.

Hata hivyo, utamaduni huu wa kuficha taarifa za afya ya rais unaonekana kuanza kuvunjwa katika miaka ya hivi karibuni.

Mbali na rais wa Nigeria Mohamadu Buhari ambae kwa miezi kadhaa yuko nchini Uingereza kwa ajili ya kupata matibabu, tumeona nchini Tanzania katika miaka ya hivi karibuni, rais mstaafu Jakaya Kikwete aliweka hadharani taarifa zake za matibabu ya tezi dume aliyopata kule nchini Marekani.

Taarifa hizo zilipokewa kwa hisia tofauti huku wengine wakihoji kwa nini taarifa hizo zimewekwa hadharani?

Lakini baadhi ya wachambuzi waliitetea hatua hiyo na kusema, wananchi walikuwa na haki ya kujua afya ya rais wao.

Bila shaka, kadri siku zinavyokwenda, na kutokana na kasi ya mitandao ya kijamii katika kueneza habari, suala la usiri halipo tena, kwani jinsi serikali itakavyojaribu kuficha taarifa hizo, lakini mara nyingi, haichukui muda mrefu bila mambo kubainika.