Uchaguzi mkuu Kenya 2017: Wasifu wa mgombea urais Joseph Nyagah

Mgombea urais, Joe Nyagah
Image caption Nyagah anasema ana ujuzi wa kutosha kuiongoza Kenya baada ya kuwa afisa wa umma kwa miaka nyingi na vile vile mwanasiasa.

Uamuzi wake Joseph Nyagah wa kujiuzulu kama mshauri wa Rais Uhuru Kenyatta mwezi Mei ili kujitosa tena katika siasa uliwaacha wengi wakijiuliza maswali mengi hasa baada ya kuchukua muda kabla ya kutangaza kiti alichokuwa analenga.

Na alipotangaza kuwa anawania urais kama mgombea huru, aliwashangaza wengi huku baadhi wakisema uamuzi wake huenda ukaonekana kama kikwazo kwa mwajiri wake wa zamani rais Uhuru Kenyatta ambaye anatafuta hatamu ya pili mamlakani.

Lakini Bwana Nyagah anasema uamuzi wake sio wa kumkwaza yeyote bali wa kuwapa Wakenya chaguo mbadala la kiongozi.

"Ukimuondoa Raila uweke Uhuru hakuna tofauti. Wakenya sasa wanataka mtu aliye huru na anayejua kazi yake. Wale hawamtaki Raila na wale hawamtaki Uhuru wataenda wapi? Hao ndio mimi natafuta, pamoja na wafuasi wao, wawili hao," anasema.

Anasema ana ujuzi wa kutosha kuiongoza Kenya baada ya kuwa afisa wa umma kwa miaka nyingi na vile vile mwanasiasa.

Bwana Nyagah alizaliwa Embu mwaka wa 1948 na kusomea shule ya msingi huko kabla ya kujiunga na shule ya Alliance. Ana shahada ya uchumi na sayansi ya siasa kutoka chuo kikuu cha Nairobi na shahada ya uzamili katika usimamizi wa fedha kutoka Chuo cha Kellogg, Chicago.

Kazi yake ya kwanza ilikuwa katika benki ya American Bank.

Alihudumu kama balozi wa Kenya katika Umoja wa Ulaya, Ubelgiji na Luxembourg kuanzia 1983 hadi 1987.

Mwaka wa 1987 aliteuliwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ndege ya Kenya Airways

Alikuwa mbunge wa Gachoka, eneo ambalo kwa sasa ni Mbeere Kusini kwa miaka 10, kuanzia 1997 hadi 2007.

Baba yake Nyagah, Jeremia Nyagah pia alikuwa waziri na mbunge wa eneo hilo la Gachoka

Huwezi kusikiliza tena
Joe Nyagah: Mimi ni mgombea asiye mfungwa uchaguzini Kenya

Nyagah alikuwa mwanachama wa KANU na waziri wa habari katika baraza la mawaziri la rais mstaafu Daniel Arap Moi hadi mwaka 2002 alipokiasi chama cha KANU na pia kujiuzulu kama waziri.

Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huo 2002 aliwania kiti cha ubunge cha Gachoka kupitia tiketi ya chama cha upinzani cha NARC.

Uamuzi wake wa kuwania urais hata hivyo sio hatua yake ya kwanza ya kisiasa ambayo inaonekana kwenda kinyume na matarajio ya wengi.

Mnamo mwaka 2007, alijiunga na kundi la viongozi watano wakuu wa chama cha ODM waliofahamika kama Pentagon na alichaguliwa kuwa waziri wa maendeleo ya ushirika na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambaye alikuwa waziri mkuu, katika serikali ya umoja wa kitaifa na rais Mwai Kibaki. Hii ni baada ya kupoteza ubunge wake kwa Mutava Musyimi

Hata hivyo, ilikuwa wakati wa kura ya maoni ya Katiba ya mwaka wa 2010 ambapo nafasi yake kama kiongozi ilijitokeza kabisa aliposhawishi jamii ya Mbeere kuunga mkono rasimu ya Katiba, wakati huu alikuwa mwenyekiti wa the Minorities Caucus katika mazungumzo ya kikatiba yaliyofanyika ukumbi wa Bomas.

Anasema kikubwa katika manifesto yake ni vita dhidi ya ufisadi kwani ndilo tatizo linalosababisha asilimia kubwa ya shida za Wakenya.

"Kenya ni nchi tajiri sana lakini tunaiba nusu kupitia mradi wa reli wa SGR, Wizara ya Afya, NYS, na kadhalika. Kila siku unasikia mabilioni yamewekwa kwa mfuko wa mtu na hatuwafuati hao wezi. Nimi nitawafuata."

Nyagah ni mmoja kati ya wagombea wanane wa kiti cha urais katika uchaguzi wa Agosti nane.

Ameifanya kampeni yake kwa kukutana na watu moja kwa moja na alikuwa miongoni mwa waliosusia mdahalo ulioandaliwa na vyombo vya habari mwishoni mwa Julai akiwa pamoja na Cyrus Jirongo, Abdouba Dida na Rais Uhuru Kenyatta.

Mada zinazohusiana