Muhubiri Gilbert Deya ashtakiwa kwa wizi wa watoto Kenya

Muhubiri Gilbert Deya
Image caption Muhubiri Gilbert Deya

Muhubiri aliyerudishwa nchini Kenya ambaye amekuwa akidai kuwapatia mimba za miujiza wanawake ameshtakiwa kwa wizi wa watoto watano nchini.

Gilbert Deya alishtakiwa kwamba kati ya mwaka 1999 na 2004 aliwaiba watoto watano mashtaka aliyokana.

Muhubiri huyo alishtakiwa katika mahakama ya Milimani saa chache tu baada ya kuwasili katika uwanja wa Jomo Kenyatta chini ya ulinzi mkali.

Wasiwasi kuhusu bwana Deya anayemiliki kanisa moja mjini London ulianza baada ya BBC kuanzisha uchunguzi 2004.

Wanawake wasio na uwezo wa kushika mimba waliohudhuria kanisa la Gilbert Deya Ministries katika eneo la Pecham, kusini mashariki mwa London waliambia kwamba wanaweza kupata watoto wa miujiza.

Lakini watoto waliibwa katika kliniki ya watoto jinini Nairobi nchini Kenya.

Bwana Deya baadaye alielekea Scotland na alikamatwa mjini Edinburgh 2006 baada ya kutolewa kibali cha kimataifa cha kumkamata kilichotolewa na Kenya.

Kanisa lake la Gilbert Deya kwa sasa linachunguzwa na tume ya hisani nchini Uingereza kwa ubadhirifu wa fedha.