Michael Wainaina: Msomi anayetaka kuongoza Kenya

Huwezi kusikiliza tena
Msomi anayetaka kuwa rais wa Kenya

Profesa Michael Wainaina ni msomi ambaye anasema aliamua kustaafu kutafuta ridhaa ya wananchi kuwa rais wa Kenya.

Anawania kama mgombea huru. Anasema alitafuta chama kinachotetea maslahi ya vijana na kina mama akakosa na ndiposa akaamua kuwa mgombea wa kujitegemea.

Profesa Wainaina, 44, ni mkazi wa kaunti ya Kiambu na ana manifesto ya nguzo 14 ambazo zinahusisha kujenga shule za talanta kote nchini Kenya ili kuwapa vijana fursa ya kukuza vipawa vyao ili kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Prof Wainaina alistaafu kama mhadhiri katika chuo kikuu cha Kenyatta mwaka wa 2013 baada ya kufanya kazi kwa takriban miaka 23.

Alianza kuandika blogu mwaka 2016 akiangazia zaidi masuala ya siasa na utawala.

Mpango wake wa kuendeleza nchi hii anasema kuwa ni kutilia maanani masuala ya vijana na mama ambao anasema wametengwa nchini.

Anaamini kuwa ni kizazi kijacho cha vijana ambacho kitaleta mabadiliko.

Na hii ndiyo azma anayosema ilimhamasisha kuingia katika kiny'ang'anyiro cha urais Kenya, ili aanzishe msingi utakaohamasisha na kuwekeza kwa vijana na kina mama ambao wataleta mwamko mpya nchini Kenya.

Shida ya ufisadi nchini, anasema, inaendelezwa na viongozi ambao kila wakiingia madarakani hufyonza rasilmali za wananchi na kuzitumia kwa manufaa yao wenyewe.

Anawanyooshea kidole cha lawama vigogo wa siasa walio katika vyama vilivyo na umaarufu zaidi nchini Kenya NASA na Jubilee ambao anasema kuwa wamefyonza maisha ya baadaye ya watoto wa Kenya kupitia siasa za ukabila na ukora.

Anawahimiza Wakenya kuwa, kama vile dawa ya kuangamiza Malaria ni kumaliza mbu wanaoeneza ugonjwa huu, basi wanaoeneza ufisadi wanafaa kuangamizwa vivyo hivyo kwa kung'atuliwa mamlakani.

Anasema iwapo atashinda urais wiki ijayo, atawapa vijana na kina mama kipaumbele kama vile Rais mstaafu wa Tanzania Julius Nyerere alivyosema kuwa dhamana ya nchi ni kuwa na vijana wenye malezi bora, siha njema na bongo kali.

Mada zinazohusiana