Mitandao ya kijamii: 'Msumeno' uliotumiwa sana uchaguzi mkuu Kenya 2017

Facebook Haki miliki ya picha Reuters

Ongezeko la watu wanaotumia mitandao ya kijamii nchini Kenya limewapatia raia wa taifa hilo ulingo wa uanaharakati wa kisiasa.

Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika Jumanne harakati hizo zimeongezeka maradufu, na ni wazi sasa kwamba ushawishi wa mitandao ya kijamii katika uchaguzi huo utakuwa mkubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Athari za mitandao ya kijamii kama nyenzo ya kuwasiliana kisiasa tayari zimeanza kuonekana kufuatia ukuaji wa mitandao hiyo kama Vile Twitter, Facebook, WhatsApp, Instagram na YouTube.

Kulingana na ripoti ya kila mwaka kuhusu hali ya mtandao nchini Kenya mwaka uliopita, kuna takriban Wakenya milioni 6.1 katika Facebook kutoka watu milioni 1.8 mwaka 2015.

Idadi ya watumiaji wa mtandao wa Twitter kila mwezi ni milioni 2.2 huku watu milioni moja wakitumia mtandao huo kila siku.

WhatsApp ni mtandao unaotumiwa sana kwa mawasiliano na unakadiriwa kuwa na watumiaji milioni 10 huku Instagram na Linkedin ikikadiriwa kuwa na watumiaji milioni 3 na milioni 1.5 mtawalia.

Wanasiasa wanajua kwamba njia ya haraka ya kueneza habari ni kuweka hoja zao na kutolipia matangazo.

Hilo limedhihirika wazi miongoni mwa wagombea wawili wakuu rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Huku Raila Odinga akionekana kuendesha mikutano yake moja kwa moja katika mitandao ya Facebook, Twitter na Instagram rais Uhuru Kenyatta amekuwa akifanya mazungumzo ya moja kwa moja na wafuasi wake katika mtandao wa Facebook.

Haki miliki ya picha Uhuru Kenyatta / Twitter
Image caption Rais Kenyatta akijibu maswali moja kwa moja kupitia Facebook akiwa ikulu, Nairobi Jumapili

Wote wamekuwa na lengo moja la kuwafikia wapiga kura vijana ambao ndio wengi miongoni mwa wapiga kura Kenya.

Raia nao pia wamepata njia rahisi ya kusikizwa na viongozi waliopo pamoja na wagombea wanapowasambazia mahitaji yao katika mitandao ya Facebook bila kupitia wasaidizi wao.

Wataalam wanasema kuwa ushawishi unaotolewa na mitandao ya kijamii katika siasa unatokana na uwezo wa mitandao hiyo kuharakisha mawasiliano na kuwafikia wapiga kura bila ya kutumia vyombo vya habari.

Huku idadi kubwa ya wapiga kura Kenya wakiwa vijana wanaotumia sana teknolojia ya kidijitali ikiwemo simu aina ya smartphones na mtandao, wagombea watakao kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi huo wa wiki ijayo watakuwa wale wanaotumia vizuri mitandao ya kijamii.

Kupitia mitandao tofauti, wana uwezo wa kufanya kampeni za mashinani mbali na kuwasihi Wakenya kujitokeza kwa wingi wakati wa shughuli ya upigaji kura.

Ubaya wa mitandao hiyo ni kwamba iwapo haitatumiwa vizuri inaweza kusababisha madhara kwa umma na kusababisha uhasama wa kikabila katika mataifa machanga kidemokrasia kama ilivyokuwa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017 nchini Kenya.

Hatahivyo matangazo hayo yamesomwa sana mitandaoni huku wengi wanaosoma wakiwa vijana hatua inayodhihirisha wazi kwamba walengwa ni vijana swala ambalo baadhi ya wachanganuzi wa mitandao kama vile Mohammed Doyo wanasema ni hatari.

"Hatari ya machapisho kama hayo ni kwamba yanawatia sumu raia, na kuwagawanya zaidi.Tayari tuna taifa ambalo limegawanyika kwa sababu nchini Kenya uchaguzi hubainiwa na maswala ya kikabila .Machapisho kama haya iwapo yataendelea kutangazwa..kwa kweli taifa hili halielekei kuzuri".

Tayari mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya, CA, pamoja na tume ya uwiano na utangamano NCIC zilisema kuwa kuna ongezeko la utumiaji wa matamshi ya chuki katika mitandao ya kijamii.

Mkurugenzi wa CA Francis Wangusi na mwenyekiti wa NCIC Francis ole Kaparo walisema kuwa ujumbe wa chuki katika mitandao ya kijamii unaweza kuligawanya taifa la Kenya katika misingi ya kikabila na hofu.

Taarifa hiyo ilisema kuwa serikali imegundua na kuzifunga akaunti 176 za mitandao ya kijamii zilizohusika katika kuchapisha matamshi ya uchochezi.

NCIC iliwaonya wasimamizi wa mitandao hiyo ya kijamii kwamba watalaumiwa kwa matamshi yoyote ya uchochezi akiongeza kuwa kesi 31 tayari zinaendelea katika mahakama tofauti nchini.

Kulingana na sheria ya NCIC 2008, mtu yeyote anayekiuka sheria hiyo atapigwa faini ya Ksh 980,000 (Dola 9,800) ama kifungo cha miaka mitatu jela.

Vilevile makosa ya kusababisha ghasia za kikabila ama zile za kibaguzi yanavutia faini ya Ksh 980,000 (Dola 9,800) ama kifungo cha miaka mitano.

Haki miliki ya picha TWITTER
Image caption Bw Odinga amekuwa akitumia sana mitandao ya kijamii kueneza ujumbe wake

Msemaji wa polisi nchini Kenya Charles Owino anasema kuwa sio rahisi kuwakamata na kuwashtaki watu.

''Huwezi kufunga mtandao wa kijamii kwa sababu utakuiwa unahujumu haki za watu na pili utakuwa unawakosesha haki yao wale wanaoutumia kwa njia ya sawa, kwa hivyo swala muhimu ni kuweka mikakati mikali na suluhu nyengine ambapo tutakuwa na uwezo kuingilia akaunti yako na kukuondoa katika mfumo mzima''.

Maafisa wa polisi hivi majuzi walimkamata na kumshtaki msimamizi wa kundi moja la WhatsApp kwa kuchochea chuki.

''Sio Vigumu kumkamata msimamizi katika kundi la WhatsApp, na kuna uwezekano mkubwa wa kumshtaki. Nakumbuka siku chache zilizopita tulikuwa na mtu mmoja aliyekamatwa mjini Eldoret kwa sababu ya vile alivyotuma ujumbe huo," alisema Charles Owino

Wanablogu, mitandao ya habari, viongozi wa kisiasa na wafuasi wao wametakiwa kuwa na busara wakati wa kipindi chote cha uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

Ijapokuwa mitandao ya kijamii inatoa huduma za haraka za kusambaza habari, haina wahariri kama inavyokuwa katika vyombo vya habari.

Hatua hiyo imesababisha kuwepo kwa habari bandia.

Hivyo basi hatua za kuthibitisha kila ujumbe ni muhimu kabla ya kuuchapisha katika mitandao hiyo.

Yote hayo ni tisa , kumi Mgombea atakayetumia vizuri huduma hizi za kidijitali ana fursa kubwa ya kuibuka mshindi .