Abduba Dida: Mwalimu anayetaka kuwa rais Kenya

Dida
Image caption Bw Dida akiwasilisha karatasi zake za uteuzi kwa tume ya uchaguzi Mei 28

Mohamed Abduba Dida ni mwalimu wa zamani ambaye aligonga vichwa vya habari Kenya alipotangaza kwamba angewania urais Machi 2013.

Wakati huo, alifahamika upesi kwa ucheshi wake na ujasiri.

Katika uchaguzi mkuu wa wakati huo, alimaliza akiwa wa nne baada ya kupata kura 52,848 ambazo ni sawa na asilimia 0.43 ya kura zilizopigwa.

Dida alizaliwa mwaka 1974 mjini Wajir kaskazini mashariki mwa Kenya.

Alikuwa mwalimu wa fasihi ya Kiingereza na dini na aliwahi kufanya kazi katika shule ya Lenana jijini Nairobi na katika shule ya upili ya Daadab katika kambi ya wakimbizi ya Daadab.

Dida ana shahada ya kwanza katika elimu kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta na shahada ya uzamili katika Elimu ya Filosofia na Dini kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alijiuzulu kazi ya ualimu mwaka 2009 ili kuangazia biashara zake.

Mwaka huu ni mara yake ya pili kuwania urais na anaamini kwamba ni yeye pekee anayeweza kutoa ushindani halisi kwa Rais Uhuru kenyatta anayewania kuchaguliwa kwa muhula mwingine uchaguzi huo wa Jumanne Agosti 8.

Anaamini pia kwamba ni yeye pekee aliye katika nafasi nzuri ya kuangamiza ufisadi nchini Kenya.

"Wagombea wengine wote hawafahamu matatizo ambayo wananchi wa kawaida wanakumbana nazo kama mimi. Nitatumia ufahamu huu kurejesha ustaarabu katika jamii," aliambia gazeti la Daily Nation mapema mwaka huu.

Dida anawania kupitia muungano wa Tunza.

Mwaka 2013, aliwania urais kupitia chama cha Alliance of Real Change.

Aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Hazina ya Maendeleo ya Maeneo bunge mwaka 2014 lakini uteuzi wake ukabatilishwa baada ya baadhi ya watu kukosoa utaratibu uliofuatwa katika kumteua.

Abdouba Dida ana wake watatu, Amina, Estail na Rukia, na watoto 11 na huwa anajivunia kuonekana hadharani na wake hao wake.

Mada zinazohusiana