Afrika Kusini: Spika aidhinisha kura ya siri kuhusu Jacob Zuma

Jacob Zuma akiwa Pietermaritzburg Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Zuma amekabiliwa na shinikizo tangu alipomfuta kazi waziri wa fedha Pravin Gordhan mwezi Machi

Wabunge nchini Afrika Kusini watapiga kura ya siri wakati wa kuamua kuhusu hoja ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma siku ya Jumanne, spika wa bunge la nchi hiyo ametangaza.

Baleka Mbete ametoa uamuzi huo baada ya vyama vya upinzani kuwasilisha kesi mahakamani wakitaka kura hiyo iwe ya siri.

Wabunge hao wanaamini kwamba iwapo kura ya siri itafanyika, wabunge wa chama tawala cha African National Congress (ANC) ambao wanampinga Zuma watakuwa na uwezekano wa juu wa kupiga kura dhidi ya rais huyo.

Bw Zuma amenusurika kura ya kotukuwa na imani naye mara kadha awali.

Chama cha ANC, ambacho kimetawala Afrika Kusini tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi wa Wazungu mwaka 1994, kina wingi wa wabunge katika bunge la nchi hiyo.

Mbunge wa ANC Makhosi Khoza amesema amepokea vitisho baada yake kutangaza kwamba angepiga kura dhidi ya Rais Zuma.

Haki miliki ya picha Reuters

Hili ndilo jaribio la karibuni zaidi la kujaribu kumuondoa madarakani Rais Zuma na linatokea baada yake kumfuta kazi waziri wa fedha aliyependwa sana na wengi Pravin Gordhan pamoja na mawaziri wengine katika mabadiliko yake kwenye baraza la mawaziri mwezi Machi.

Rais huyo amekabiliwa na tuhuma za kujihusisha katika ufisadi na kwamba amekuwa na uhusiano na familia ya matajiri ya Gupta, ambao wanadaiwa kuwa na ushawishi wakati wa maamuzi yake ya kisiasa.

Bw Zuma na familia ya Gupta wote wamekanusha tuhuma hizo.

Mwezi Juni, majaji wa Mahakama wa Kikatiba waliamua kwamba Bi Mbete ana mamlaka ya kufanya uamuzi kuhusu iwapo wabunge wapige kura ya siri.

Mada zinazohusiana