Uchaguzi 2017: Kenya yasubiri uchaguzi wenye ushindani mkali

Ezra Chiloba
Image caption Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Ezra Chiloba amesema tume hiyo iko tayari kwa uchaguzi mkuu Jumanne

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Kenya (IEBC) imetangaza kwamba iko tayari kwa uchaguzi mkuu ambao utafanyika Jumanne nchini humo.

Tume hiyo hata hivyo imesema uchaguzi huo unaweza kuathirika iwapo changamoto za kiusalama hazitatatuliwa.

Jumla ya wapiga kura 19 milioni wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo, ambapo watamchagua rais, wabunge, maseneta, magavana, wawakilishi wa wanawake na wawakilishi wa wadi.

Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa kumi na mbili alfajiri na kufungwa saa kumi na moja jioni.

Tume imesema usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi ungekamilika baadaye leo jioni.

Maandalizi ya uchaguzi huo yaliingia doa baada ya kuuawa kwa meneja wa masuala ya teknolojia katika tume ya uchaguzi Chris Msando wiki moja kabla ya uchaguzi.

Afisa mkuu mtendaji wa IEBC Ezra Chiloba ameambia BBC kwamba wanafanya kazi kwa karibu sana na maafisa wa usalama kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa njia salama.

Bw Chiloba amesema maafisa wa uchaguzi watalindwa na maafisa wa usalama na kwamba kutakuwa pia na maafisa wa kutosha wa usalama vituoni kuhakikisha wapiga kura wanashiriki uchaguzi kwa njia ya amani.

Katika mji wa Kisumu, magharibi mwa Kenya, baadhi ya raia wamelalamika kwamba hawajapata majina yao katika orodha ya wapiga kura vituoni.

Jumla ya watu 300 waliandamana hadi afisi za tume hiyo kulalamika kwamba majina yao hayakuwa kwenye orodha ya wapiga kura licha ya kwamba walijiandikisha kuwa wapiga kura na kwamba walihakiki pia taarifa kuhusu usajili wao.

Image caption Baadhi ya wapiga kura Kisumu wamesema hawapati majina yao katika orodha ya wapiga kura

Bw Chiloba hata hivyo amesema wengi wa wapiga kura hawakutumia fursa iliyotolewa ya kuhakiki maelezo yao kwenye sajili ya wapiga kura.

Amesema kati ya wapiga kura milioni 19 waliojiandikisha, ni wapiga kura milioni saba pekee waliotumia fursa hiyo.

Kuna wagombea wanane katika kinyang'anyiro cha urais.

Wachanganuzi wanasema ushindani mkubwa ni kati ya Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa).

Hii ni mara ya nne kwa Bw Odinga kuwania urais.

Mwaka 2013, aliwania kupitia muungano wa Coalition for Reform and Democracy (Cord) lakini akashindwa na Bw Kenyatta.

Huwezi kusikiliza tena
Mambo muhimu kuhusu uchaguzi wa urais Kenya 2017
Image caption Wananchi wakitafuta majina yao katika orodha ya majina ya wapiga kura Eldoret
Image caption Maafisa wa usalama wakishika doria mjini Eldoret, magharibi mwa Kenya

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii