Kenyatta kwa Wakenya: Mkipiga kura nendeni nyumbani

Rais Kenyatta Haki miliki ya picha Uhuru Kenyatta / Facebook
Image caption Kenyatta ametoa hotuba yake ya mwisho kabla ya uchaguzi mkuu Jumanne

Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa wapiga kura nchini humo kuondoka kwenye vituo vya kupigia kura na kwenda nyumbani baada ya kupiga kura.

Kiongozi huyo, katika hotuba kwa taifa kabla ya uchaguzi mkuu Jumanne, amesema wananchi wanafaa kupiga kura kwa amani.

"Ombi langu ni kwamba tunapopiga kura, hebu tupige kura kwa amani na tukumbuke kama nilivyosema jana, kwamba baada ya kupiga kura yako, nenda nyumbani. Nenda kwa jirani yako," amesema.

"Bila kujali anatoka wapi, kabila lake, rangi au dini, jirani yako ni ndugu yako. Jirani yako ni dadako.

"Jinsi ulivyopiga kura haifai kwa vyovyote vile kuathiri au kubadilisha jinsi unavyohusiana na jirani yako.

"Msalimie kwa mkono, kuleni chakula pamoja na uwaambie 'hebu tusubiri matokeo' kwani Kenya itaendelea kuwepo kwa muda mrefu hata baada ya uchaguzi."

Muungano wa upinzani ulikuwa awali umewashauri wafuasi wake kutoondoka vituo baada ya kupiga kura 'kulinda kura'.

Lakini baadaye, muungano huo ulibadilisha wito wake na kuwashauri waondoke baada ya kupiga krua lakini warejee baadaye jioni.

Polisi wamewataka wananchi kuheshimu sheria ya kutokuwa karibu na vituo vya kupigia kura umbali wa mita 400 baada ya kupiga kura.

"Wazazi wetu walipigana ndipo tuwe na Kenya nzuri na maisha mazuriā€¦bila kujali matokeo ya uchaguzi huu, ni lazima tuendelee kushikamana pamoja kama wananchi. Zaidi ya yote, tukatae kutishwa. Lazima tukatae ghasia au majaribio yoyote ya kutugawanya," amesema Bw Kenyatta.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii