Uchaguzi Kenya2017: Je fomu 34A na 34B ni zipi?

Chini ya sheria ya uchaguzi, fomu 34A ndio fomu ya kwanza inayotumika kunakili matokeo ya uchaguzi wa urais
Image caption Chini ya sheria ya uchaguzi, fomu 34A ndio fomu ya kwanza inayotumika kunakili matokeo ya uchaguzi wa urais

Kukataliwa kwa matokeo ya uchaguzi katika tovuti ya tume ya uchaguzi nchini Kenya kwa mara nyengine tena kumezua majina ya fomu zinazotumiwa katika kunakili matokeo ya uchaguzi.

Fomu zilizotajwa na mgombea wa upinzani wa Nasa Raila Odinga ni zile za 34A na 34B.

Katika kuyakataa matokeo hayo ya IEBC katika mtandao wake bwana Odinga alisema kuwa fomu 34A na 34B lazima zitolewe.

IEBC imesema kuwa maajenti wa mgombea huyo wa urais wataonyeshwa fomu 34A.

Je hizi ni fomu gani?

Chini ya sheria ya uchaguzi, fomu 34A ndio fomu ya kwanza inayotumika kunakili matokeo ya uchaguzi wa urais.

Fomu hiyo hujazwa na afisa wa tume ye uchaguzi anayesimamia uchaguzi huo kwa jina la Presiding officer baada ya kuhesabiwa kwa kura katika kituo cha kupigia kura.

Fomu hiyo huwa na maelezo kuhusu kura zilizohesabiwa za kila mgombea mbali na kuwa na idadi ya wapiga kura katika kituo hicho, kura zilizoharibika, zile zilizo na utata na kura zilizokubalika.

Mgombea ama ajenti wake baadaye hutakiwa kutia saini ili kuthibitisha kwamba yaliomo ndani ya fomu hiyo ni sahihi.

Kifungu cha 39 cha uchaguzi kinasema kuwa ili kufanyika kwa uchaguzi wa urais tume ya uchaguzi itatoa matokeo hayo kielektroniki baadaye kuyasafirisha kutoka katika kituo cha kupigia kura hadi katika kituo cha kuhesabia kura cha eneo bunge na baadaye katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura.

Form 34A hupewa afisa anayesimamia uchaguzi katika eneo bunge ambaye hujaza fomu 34B.

Hutumika kuonyesha matokeo ya kura ya urais.

Fomu hiyo huonyesha nambari ya kituo cha kupigia kura, jina la kituo cha kupigia kura, idadi ya watu waliojisajiliwa kupiga kura katika kituo hicho, matokeo ya kila mgombea na idadi ya kura zilizokubalika.

Afisa anayesimamia shughuli ya uchaguzi katika eneo bunge kwa jina Returning officer humpelekea fomu hiyo mwenyekiti wa tume ya auchaguzi IEBC ambaye ndio afisa mkuu wa matokeo ya uchaguzi wa urais.

Katika mkutano na vyombo vya habari makamu wa mwenyekiti wa tume ya IEBC Consolata Maina amesema kuwa fomu hiyo ndio itabaini ni nani mshindi wa kura ya urais.

Sheria inaruhusu kuipata fomu 34B kutoka kwa kila Retuning officer kabla ya kutangaza matokeo.

''Utangazaji wa matokeo unategemea fomu 34B ambayo tutapata kutoka kwa Retuning Officers'', alisema bi Maina.