Mama amshinda mwanawe uchaguzi wa ubunge Kenya

Beatrice Kones
Maelezo ya picha,

Bi Kones aliingia bungeni mara ya kwanza kupitia uchaguzi mdogo mwaka 2008

Katika siasa, mambo ya kipekee hutokea. Hebu tafakari wakati mtoto ambaye bado anaishi na mama yake anakuwa mpinzani wake. Nani atashinda?

Katika eneo bunge la Bomet Mashariki, katika kaunti ya Bomet kusini mwa uliokuwa mkoa wa Bonde la Ufa, hali hiyo ilijitokeza.

Mbinge wa zamani Beatrice Kones, mjane wa waziri wa zamani Kipkalya Kones aliyewania kupitia chama cha Jubilee alikabiliana na wagombea wengine 8 akiwemo mtoto wake wa kiume Kipngetich Kones.

Bw Kones aliwania kupitia chama kinachoegea upande wa upinzani wa Chama cha Mashinani (CCM).

Kulikuwa na ushindani mkali ulioiacha familia ikiwa imegawanyika.

Bi Kones alishinda kiti hicho cha ubunge mara ya kwanza kwenye uchaguzi mdogo, kufuatia kifo cha mumewe mwaka 2008 na akahudumu hadi mwaka 2013.

Wakati wa kampeni mtoto wake alimshutumu mara kwa mara mama yake kuwa kukosa mipango mipya ya kuwanufaisha watu wa Bomet Mashariki.

Lakini wapiga kura waliamua kumchagua mama.

Bi Kones amepata kura 22,796 ambazo ni sawa na asilimia 53.57 ya kura zilizopigwa.

Wa pili alikuwa mgombea wa kujitegemea Bernard Bett aliyekuwa na kura 12,042.

Bw Kones alimaliza wa nne akiwa na kura 2,410, sawa na asilimia 5.66.