Aliyekuwa mlinzi wa mbunge achaguliwa kuwa mbunge Kenya

Nimrod Mbithuka Mbai wakati mmoja aliwahi kuwa mlinzi wa wabunge na maafisa wa serikali Haki miliki ya picha Nation media
Image caption Nimrod Mbithuka Mbai wakati mmoja aliwahi kuwa mlinzi wa wabunge na maafisa wa serikali

Nimrod Mbithuka Mbai wakati mmoja aliwahi kuwa mlinzi wa wabunge na maafisa wa serikali, lakini baada ya kupata ushindi wa uchaguzi wa Agosti 8 sasa atahudumu kama mbunge kwa kitui mashariki.

Gazeti la Daily Nation nchini Kenya limesema kuwa afisa huyo wa zamani wa polisi alimshinda mbunge aliyepo madarakani na sasa atajiunga na mbunge aliyekuwa akimlinda bungeni baada ya wote wawili kuchaguliwa katika bunge jipya.

Alipata kura 14,256 dhidi ya mpinzani wake wa karibu aiyepata kura 10,899.

Bwana Mbai alihudumu kama mlinzi wa aliyekuwa msemaji wa zamani wa serikali kabla ya kujiuzulu kama polisi.

Kama mlinzi, kazi yake ya kila siku ilikuwa kuandamana na wanasiasa kwa kazi za kiserikali ikiwemo mikutano ya hadhara na kutumia muda wao mrefu wakiwa ndani ya gari huku wanaowalinda wakiwa katika mikutano mara nyengine hadi usiku wa manane.

Na sasa mtu mwengine atakuwa akimlinda bwana Mbai kufanya kazi ,kwa kumfungulia mlango wa gari na kumlinda.