Charlottesville: Trump ashutumiwa kuhusu mkutano wa Wazungu wababe

Mamia ya Wazungu watetezi wa ubabe, Wanazi mambo leo na watu wa mrengo wa kulia walikabiliana na waandamanaji waliopinga mkutano Charlottesville - 13 August Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mamia ya Wazungu watetezi wa ubabe, Wanazi mambo leo na watu wa mrengo wa kulia walikabiliana na waandamanaji waliopinga mkutano Charlottesville

Rais wa Marekani Donald Trump ameshutumiwa vikali kutokana na alivyojibu ghasia zilizozuka katika mkutano wa watetezi wa ubabe wa Wazungu nchini Marekani.

Mwanamke mmoja aliuawa na watu wengine 19 wakajeruhiwa baada ya gari kuvurumishwa kwenye waandamanaji wa kupinga mkutano huo uliofanyika Charlottesville, Virginia.

Bw Trump alishutumu ghasia za "pande nyingi" - lakini hakushutumu moja kwa moja watu wa mrengo wa kulia walioandaa mkutano huo.

seneta wa Republican Cory Gardner amesema "Bwana Rais - ni lazima tuutaje uovu kwa jina lake."

Aliongeza: "Hawa walikuwa wanatetea ubabe wa Wazungu na huu ni ugaidi wa ndani."

Matamshi yake yaliungwa mkono na maafisa wengine wakuu wa chama cha Republican chake Rais Trump.

Mamia ya watu wanaotetea ubabe wa Wazungu walikusanyika kwa maandamano hayo ya Jumamosi yaliyopewa jina "United the Right" (Unganisha mrengo wa Kulia). Walikuwa wanapinga kuondolewa kwa sanamu ya shujaa mtetezi wa kujitenga kwa majimbo ya kusini.

Waandamanaji hao waliojumuisha pia makundi yanayounga siasa za ki-Nazi na wanachama wa Ku Klux Klan, walikabiliana na waandamanaji waliokuwa wanapinga mkutano huo.

Watu walipigana kwa mangumi na mateke, huku gesi ya pilipili ya kuwasha ikitumiwa na pande zote mbili.

Mkutano huo ulipokuwa unakomeshwa, gari lilivurumishwa kwenye waandamanaji wa kupinga mkutano huo.

Gari hilo liliwagonga na kuwarusha watu juu.

Kijana James Fields wa miaka 21 kutoka jimbo la Ohio, ambaye anadaiwa kwua dereva wa gari hilo, amekamatwa na kuzuiliwa kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya ngazi ya pili.

Maafisa wa FBI wameanzisha uchunguzi.

Kando na mauti na majeruhi kutokana na kisa hicho cha gari, polisi wa Charlottesville wamesema watu wengine zaidi ya 15 walijeruhiwa katika ghasia zilizohusiana na maandamano hayo.

Gavana wa Virginia, Terry McAuliffe, alisema ujumbe wake pekee kwa Wazungu wababe waliokuwa wamefika Charlottesville ni kwamba "Waende nyumbani kwao".

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mwandamanaji wa mrengo wa kulia akiwa na ngao ya kujikinga

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii