Uchaguzi Kenya: Odinga achelewa kutangaza hatua atakayochukua

Bw Odinga na Bw Mudavadi Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bw Odinga na Bw Mudavadi

Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) umeahirisha kikao cha kutoa tangazo kuhusu mweleko wa chama hicho kufuatia uchaguzi mkuu wa Jumanne wiki iliyopita.

Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga alikuwa ameahidi kwamba angetangaza ni hatua gani atachukua leo baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa Ijumaa, ambapo mpinzani wake Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.

Ajenti mkuu wa Nasa Musali Mudavadi amesema sasa muungano huo unapanga kutoa tangazo kesho Jumatano.

"Tunasikitika kwamba mashauriano yanachukua muda mwingi kuliko ilivyotarajiwa na Nasa kwa hivyo hawataweza kuwahutubia Wakenya kama walivyotarajia leo."

Bw Mudavadi hata hivyo amesema mashauriano "yanaendelea na yanaendelea vyema".

Rais Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.

Hapo jana, Bw Odinga alikuwa ametoa wito kwa wafuasi wake kususia kazi kabla ya kutoa tangazo kubwa leo.

Watu wengi hata hivyo walionekana kupuuza wito wa kususia kazi.

Baada ya kutokea kwa maandamano katika baadhi ya maeneo ambayo ni ngome ya upinzani mitaa ya Mathare na Kibera jijini Nairobi na mji wa Kisumu, hali ya utulivu ilianza kurejea Jumatatu.

Viongozi wa muungano huo wa upinzani wanadai mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ilidukuliwa na watu wenye uhusiano na serikali ya Jubilee na kwamba watu hao waliingilia na kuchakachua matokeo kumfaa Rais Uhuru Kenyatta aliyekuwa akishindana na Bw Raila Odinga kwa mara ya pili.

Tume ya uchaguzi ilisema mwanzoni ilikuwa haina taarifa kuhusu udukuzi kama huo lakini kwamba ingelifanya uchunguzi. Saa chache baadaye, tume hiyo ilisema hakuna jaribio lolote la udukuzi lililokuwa limefanyia katika sava ya matokeo ya uchaguzi.

Muungano wa upinzani pia umeikosoa IEBC kwa kutoa matokeo ya urais bila kuwasilisha fomu za kutangazwa kwa matokeo katika vituo vya kupigia kura na pia katika maeneo bunge, Fomu 34A na Fomu 34B.

Muungano huo umesema hautaenda kortini kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii