Rais wa Misri awasili Rwanda kwa mazungumzo ya kibiashara

Sisi
Image caption Rais Al Sisi alifika Rwanda baada ya ziara ya kikazi nchi jirani ya Tanzania

Rais wa Misri Abdel Fatah Al Sisi ameanza ziara ya siku mbili nchini Rwanda.

Mbali na masuala ya siasa, kiongozi huyo na mwenyeji wake Paul Kagame wanatarajiwa kuzungumzia ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na kutia saini mikataba ya kibiashara na uwekezaji.

Ziara ya Rais Al Sisi hapa nchini imeanzia eneo la Gisozi kwenye jumba la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambako ameweka shada la maua kutoa heshima zake kwa masalio ya miili ya watu waliouawa katika mauaji hayo kabla ya kuwa na mazungumzo na Rais Kagame.

Hakuna mengi yaliyotangazwa kuhusu ratiba nyingine ya ziara ya rais Al Sisi nchini Rwanda.

Misri na Rwanda zina uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia.

Mbali na siasa, ziara hii inataraji kujikita zaidi kuhusu ushirikiano kibiashara na uwekezaji.

Misri ni miongoni mwa nchi za kwanza barani Afrika kuwekeza katika nchi za kigeni kitita cha bilioni 6.8 dola za Marekani.

Upande wa Rwanda, nchi hiyo tayari imekwishawekeza katika miradi ya usambazaji wa maji ikizingatiwa kwamba asilimia 85 ya maji inayotumia ni ya Mto Nile ambao una baadhi ya vyanzo vyake nchini Rwanda.

Mwaka jana Rwanda ilichota kitita cha dola milioni 26 za Marekani kwa biashara ya kahawa, chai na maua inayofanya na Misri huku Misri ikiingiza dola milioni 54 kwa bidhaa inazouza Rwanda hususanivifaa vya ujenzi.

Katika ziara hii mikataba zaidi hasa ya uwekezaji inataraji kutiwa saini, miongoni mwake ni kuifungulia milango kampuni ya ndege ya Egyptair kufanya safari zake Rwanda kufuatia mwafaka ulioafikiwa mwaka 2015 lakini ukawa haujatekelezwa.

Ziara ya Rais Al Sisi aliyoanzia nchini Tanzania itampeleka pia katika nchi za Chad na Gabon.

Haki miliki ya picha Ikulu, Tanzania
Image caption Al Sisi akiagana na Rais wa Tanzania John Magufuli mapema leo

Kisiasa inaangaliwa kama nchi hiyo ya kiarabu inataka ufungamano zaidi na nchi za maeneo ya Afrika ya kusini mwa jangwa la Sahara na hasa kuwa na sauti katika Umoja wa Afrika ambao kuanzia mwakani utaongozwa na Rais Kagame.

Nchini Tanzania, Rais al-Sisi alikubali kujenga kiwanda kikubwa cha nyama ili kuwawezesha wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao.

Aidha, alikubali kujenga kiwanda cha dawa za binadamu. Tanzania huagiza kutoka nje ya nchi dawa za binadamu kwa asilimia 100.

Mada zinazohusiana