Waangalizi waitaka IEBC kuchapisha fomu 34A Kenya

Aliyekuwa waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry aliwakilisha kituo cha Carter Center katika uchaguzi wa Kenya
Image caption Aliyekuwa waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry aliwakilisha kituo cha Carter Center katika uchaguzi wa Kenya

Kituo cha Carter Centre kilichoshiriki katika uangaliza wa uchaguzi mkuu uliokamilika nchini Kenya sasa kimeitaka tume ya uchaguzi nchini humo IEBC kuharakisha uchapishaji wa matokeo ya uchaguzi ya fomu 34A.

Kituo hicho kimesema IEBC inafaa kufanya hivyo haraka iwezekanavyo kikitaja siku ya mwisho ya tarehe 18 mwezi Agosti ambapo wale wanaopinga matokeo ya uchaguzi huo watawasilisha pingamizi zao mahakamani.

Kimesema kuwa uchapishaji wa matokeo ya kila kituo cha kupigia kura ni njia inayotambulika kimataifa ili kuhakikisha kuwa kuna uwazi katika shughuli nzima ya uchaguzi mbali na kuwa uma una imani na matokeo hayo.

''Ni muhimu kwa wanaotaka kuwasilisha pingamizi zao kuwa na uwezo wa kutazama data ya matokeo hayo ili kuweza kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kupitia mahakama'', ilisema taarifa hiyo.

Hatua hiyo inajiri baada ya IEBC kutoa tangazo hapo jana kwamba tayari imekamilisha uchapishaji wa fomu zote 290 za 34B.

Kulingana na Kituo hicho IEBC bado haijachapisha fomu zote za matokeo ya 34A kutoka katika vituo vya kupiga kura.

Wakati huohuo kituo hicho kimeshutumu maafa yaliotokea wakati na hata baada ya uchaguzi kufuatia kutangazwa kwa matokeo.

Waangalizi hao wamemtaka inspekta jenerali wa polisi kuwalinda Wakenya na haki zao.

Aidha kimewataka maafisa hao wa usalama kukoma kutumia nguvu nyingi na kuwalinda Wakenya wanaotumia haki zao za kikatiba kujieleza.

''Tunaisihi serikali kuhakikisha kuwa wale walioathirika katika ghasia hizo wanapata matibabu na usaidizi wa kibinaadamu huku uchunguzi wa kutumia nguvu kupitia kiasi uliotekelezwa na polisi ukifanywa''.

Vilevile kituo hicho kimesema kuwa kina wasiwasi kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka nchini Kenya kupiga marufuku mashirika yasiokuwa ya kiserikali ambayo yamejihusisha na shughuli ya kupiga kura ya Kenya.

Mashirika hayo ni Human Rights Commission na lile Africa Centre for Open Governance {africog}.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari waangalizi hao wa uchaguzi wamesema kuwa haki za Wakenya kushiriki katika maswala ya umma ni jambo muhimu katika jamii ya kidemokrasia ambapo serikali ina jukumu la kulinda.

Hatahivyo waangalizi hao wamesema kuwa wanaunga mkono hatua ya waziri wa maswala ya ndani kufutilia mbali hatua hizo na kushirikiana na mashirika hayo ili kuafikiana kuhusu utendaji wao.

Mada zinazohusiana