Msichana wa miaka 10 aliyebakwa India ajifungua

A protest in India against child sex abuse Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano ya kupinga dhuluma za kingono dhidi ya watoto India

Msichana wa umri wa miaka 10 ambaye alinyimwa ruhusa ya kuavya mimba na mahakama ya juu zaidi nchini India mwezi uliopita amejifungua mtoto msichana.

Msichana huyo hajafahamu kuwa amejifungua. Wakati akiwa na uja uzito aliambiwa kuwa tumbo lake kubwa lilitokana na jiwe kubwa lililokuwa ndani ya tumbo.

Mtoto huyo mwenye uzito wa kilo 2.5 alizaliwa kwa njia ya upasuaji katika hospitali ya Chandigarh.

Mama na mtoto wote wako hali nzuri, afisa mmoja aliiambia BBC.

Msichana huyo anadaiwa kubakwa mara kadha katika kipindi cha miezi saba iliyopita na mjomba wake ambaye wa sasa amekamatwa.

Mimba yake iligunduliwa karibu mwezi mmoja uliopita wakati alilalamikia maumivu ya tumbo na wazazi wake wakampeleka hospitalini.

Mwezi uliopita mahakama ya juu ilikataa kumruhusu kuavya mimba hiyo kwa misingi kuwa alikuwa mdogo sana kuwa mjamzito, baada ya madaktari kusema kuwa kuavya mimba hiyo ya wiki 32 yaweza kuhatarisha maisha yake.

Mada zinazohusiana