Mwanzo wa mwisho wa dunia utakuwa Jumatatu 21 Agosti?

Jua litapatwa na mwezi kikamilifu Amerika kaskazini kwa mara ya kwanza kabisa Jumatatu tangu 1918 Haki miliki ya picha Alamy
Image caption Jua litapatwa na mwezi kikamilifu Amerika kaskazini kwa mara ya kwanza kabisa Jumatatu tangu 1918

Mnamo Jumatatu tarehe 21 Agosti, tukio lisilo la kawaida litashuhudiwa Amerika Kaskazini, ambalo limewavutia watu zaidi ya milioni saba wanaotarajia kulishuhudia katika miji mbalimbali Marekani.

Kwa mara ya kwanza tangu 1918, jua litapatwa kikamilifu na mwezi Marekani.

Bara lote la Amerika Kaskazini litafunikwa na giza totoro mchana.

Ingawa baadhi ya watu wanalitazama tu kama tukio la kuvutia, kwa wengine, hili linaashiria mwisho wa dunia kama tunavyoifahamu kwa sasa.

Makundi mbalimbali ya Kiinjilisti nchini Marekani kwa mfano, yameanza kuhubiri kwamba tukio hilo linaashiria kukaribia kwa mwisho wa dunia.

Tovuti moja ya unabii wa Kikristo kwa jina Unsealed imedai kwamba tukio hilo la Jumatatu litaanzisha kipindi cha Majonzi, kipindi cha miaka saba ambapo katika kipindi hicho asilimia 75 ya watu wote duniani wataangamizwa.

Kwa wengine hata hivyo, ni tukio ambalo wamesubiri sana kwa hamu majira haya ya joto.

Kuna watu 12 milioni ambao wanaishi eneo la upana wa maili 70 9kilomita 112) kutoka Oregon hadi Carolina Kusini ambapo mwezi utalifunika kabisa jua.

Utalii wa "kutazama kupatwa kwa jua" unatarajiwa kuwazolea pesa nyingi sana, utalii ambao ulianza kupata umaarufu karne ya 18 ambapo watu wengi walisafiri hadi miji ambayo jua lingepatwa na mwezi Ulaya.

Lakini ni kwa nini tukio hili nadra sana linavutia watu wengi na pia kwa wengine kuibua wasiwasi?

Wasiwasi zama za kale

Katika karne ya 7 kabla ya kuzaliwa kwa yesu Kristo, mshairi maarufu Archilocus aliandika kuhusu kutokea kwa tukio hilo katika ksiiwa cha Paros, Ugiriki: " Hakuna jambo linaloweza kunishangaza tena duniani sasa. Kwani Zeus, babake Olympian, amegeuza mchana kuwa usiku wa giza kwa kulifunika jua, na sasa ukatili wa giza unawakodolea macho binadamu. Jambo lolote linaweza kutokea."

Haki miliki ya picha Alamy
Image caption Tangu zamani tukio la jua kupatwa na mwezi limekuwa likizua wasiwasi wa mwisho wa dunia

Watu wengi hawakufahamu kabisa nini kilitokea wakati wa jua kupatwa na mwezi, hadi karne ya 17, anasema Edwin Krupp, mkurugenzi wa kituo cha kutafiti anga za juu cha Griffith jimbo la California.

Wagiriki hawakuwa peke yao katika kuingiwa na wasiwasi.

Ingawa kuna wasomi kadha kuanzia karne ya 8 tangu kuzaliwa kwa Yesu ambao walianza kufahamu jua hupatwa vipi na mwezi, kwa miaka mingine 2,000, watu wengi duniani walihusisha tukio hilo na miungu.

Krupp anasema kwa muda mrefu, watu walijaribu kufafanua yaliyokuwa yakitokea na mambo na vitu vilivyowazunguka.

Hadi wa leo, baadhi ya maeneo duniani bado kuna itikadi kuhusu tukio la mwezi jua kupatwa na mwezi.

Nchini India, kuna baadhi ya wajawazito hawawezi kutoka nje ya nyumba zao wakati wa tukio hilo kwa sababu wanaogopa wanaweza kupatwa na madhara.

Ili kukabiliana na wasiwasi huo, baadhi ya jamii zilianza kufanya matambiko, wakijaribu kuwasiliana na nguvu au mashetani ambao waliamini walihusika katika kuliziba jua.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption "Tubuni; kwani Ufalme wa Mungu unakaribia," unasoma ujumbe katika bango hili lililobebwa na mmoja wa wanaoamini mwisho wa dunia unafika mjini Washington DC mwezi jana.

Moja ya itikadi za wakati huo ni kwamba kulikuwa na nduli aliyekuwa anashambulia Jua au Mwezi.

Asia magahribi, watu waamini jua kupatwa na mwezi kulitokana na zimwi kulishambulia jua. Wangepiga ngoma kubwa kujaribu kumtia woga nduli huyo aliache jua. China waliamini mbwa ndiye alikuwa analishambulia jua. Peru nako, wakazi waliamini mnyama mkubwa aina ya puma ndiye aliyekuwa analishambulia jua. Ulaya, maharamia wa Scandinavia maarufu kama Viking waliamini mbweha angani wlaikuwa wanashambulia jua. Si ajabu kwamba neon la kale zaidi kuhusu jua kupatwa na mwezi nchini China ni shih, ambalo lina maana ya "kula".

'Mapenzi ya Jua na Mwezi

Si watu wote hata hivyo walioogopa tukio hilo. Watu wa jamii ya Batammaliba nchini Togo na Benin walikuwa wakitazama tukio hilo kama vita kati ya Juan a Mwezi. Wangewahimiza kuacha vita na kutumia wakati huo kumaliza uhasama wa tangu jadi na kusameheana. Watu asilia wa kusini mwa Pasifiki na Amerika kaskazini magharibi walitazama tukio hilo kama wakati wa mapenzi. Waliamini Jua na Mwezi zilikuwa zinajificha nyuma ya pazia kushiriki mahaba faraghani.

Jarita Holbrook, mtaalamu wa anga za juu, anasema watu walitazama tukio hilo kwa kutegemea utamaduni wao. Katika maeneo ambayo kuna joto na chakula, miungu si wakatili na hivyo unalitazama kwa upande wa mema.

Lakini iwapo utamaduni wenu una dini ambapo miungu wanawatazama na wanaweza kuwaadhibu, basi utaogopa tukio kama hilo na kulihusisha na maafa "na mwisho wa dunia."

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Ulaya nyakati za Ukristo. Baada ya kuhangaishwa na tauni, vita na pia baada ya kufahamu vyema Biblia, fikira zao wakati wa tukio la jua au mwezi kupatwa zilikimbilia katika kitabu cha Ufunuo ambacho kinatabiri wakati ambapo Jua litageuka na kuwa giza nao mwezi ubadilike na kuwa rangi ya damu.

"Ni rahisi sana kuelewa ni kwa nini watu hufikiria hivi," anasema Chris French, profesa anayeangazia masuala ya saikolojia.

"Kitendo cha Jua kutoweka angani wakati wa jua kupatwa na wezi, kuna mambo mengi kiishara yanayohusishwa na hilo. Wakati wa mweiz kupatwa na jua, jua hugeuka na kwua rangi nyekundu. Na unagaa kukumbuka kwamba kwa watu wengi, hili ni jambo ambalo hawajawahi kuliona. Muda wa kuishi ni mfupi, na kwa hivyo haya si matukio ya kawaida."

Wahispania walipoteka himaya ya Aztec katika karne ya 16, kulikuwa na mtawa wa kundi la Francisca kwa jina Bernardino de SahagĂșn, ambaye sasa hcuhukuliwa kama mmoja wa wanaanthroporojia wa kwanza kabisa.

Anazungumzia wenyeji walivyopokea tukio la jua kupatwa na mwezi:

"Wote waliingiwa na wasiwasi na kuanza kulia. Watu wa kawaida walilia, kwa sauti. Kelele zilitanda kote. Watu wa rangi ya maji ya kunde walichinjwa kama kafara. Mateka waliuawa. Wote walitoa damu zao. Katika mahekalu yote, watu waliimba na kucheza zaburi. Kulikuwa na nyimbo za vita. Baadhi walsiema, iwapo hii itakamilika, basi kutakuwa na giza daima. Mashetani wa giza watashuka na kuwala binadamu."

Nguvu za kisiasa

Kwa watu wachache waliofahamu kilichokuwa kinaendelea, walitumia tukio hilo kujifaa kisiasa.

Mwaka 1504, wanabaharia wake walipokuwa karibu kufa njaa baada ya meli yao kuzama pwani ya Jamaica, Christopher Columbus alikomesha maasi kwa kutumia tukio la mwezi kupatwa na jua kuwafanya wenyeji wa jamii ya Arawak kwamba alikuwa amedhibiti mbingu. Aliwashurutisha kumpa chakula.

Miaka 300 baadaye, alipokuwa anaunga ufalme wa Wazulu, Shaka kaSenzangakhona aliimarisha utawala wake kwa kuwashawishi watu wake kwamba alikuwa na uwezo wa kulidhibiti jua.

Moja ya sababu ambazo hufanya imani ya mambo kutokea kutokana na jua kupatwa na mwezi ni sadfa tu.

Kwa watu ambao wanaamini katika nguvu za nyota na unajimu, na kwamba mpangilio wa nyota huwa na ujumbe fulani, bila shaka kutakuwa na sadfa ambapo tukio la watu kuona kimondo na kifo cha mtu au kuzaliwa kwa moto vitatokea wakati mmoja.

French anasema kwa wale ambao hawaamini mambo kama hayo yanaweza kutokea kwa pamoja kwa kawaida, hilo huwapa sababu zaidi ya kuamini katika unajimu.

Sababu nyingine ni kwamba miili ya binadamu hubadilika kutokana na tukio lisilo la kawaida mfano jua kupatwa na mwezi.

Holbrook anasema. "Mapigo ya moyo wako huongezeka, kuna mabadiliko katika kiwango cha joto mwilini, kupumua, mboni za macho na pia kutokwa na jacho. Kunao wanaoamini kwamba hili hutokea kwa sababu binadamu huzaliwa na uwezo asilia wa kutambua yanayojiri duniani, na unapokumbana na jambo ambalo kawaida huwa haliwezekani, hilo huufanya ubongo kchukua hatua."

"Miili yetu huchukua hatua kwa njia sawa, lakini jinsi hayo hufasiriwa hutegemea utamaduni."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii