Mawakili kupinga kinga ya kidiplomasia ya Bi Mugabe

Bi Mugabe na mkewe Grace Mugabe
Image caption Bi Mugabe na mkewe Grace Mugabe

Wakili wa Gabriela Engels, mwanamitindo wa Afrika Kusini ambaye alidaiwa kupigwa na mke wa Mugabe bi Grace Mugabe ameambia BBC kwamba atawasilisha ombi katika mahakama kuu mjini Pretoria kukabiliana na kinga ya kidiplomasia iliopewa bi Mugabe.

Willie Spies aliambia BBC kwamba mawakili wa bi Engels wanakichukulia kisa hicho kama unyanyasaji kwa lengo la kutaka kumjeruhi mteja wao.

Aliongezea kuwa bi Mugabe hafai kupewa kinga hiyo ya kidiplomasia na kwamba serikali ya Afrika Kusini ilikiuka sheria.

''Sheria zetu kuhusu kinga za kidiplomasia ziko wazi. Moja inasema kuwa sheria hiyo haifai kutumiwa iwapo mtu amejeruhiwa na kwamba haifai kutumiwa iwapo uhalifu mbaya umefanyika.Kupiga mtu kwa lengo la kumjeruhi ni uhalifu''.

Anasema kuwa mawakili wa bi Engels wataliangazia ombi hilo mahakamani ili kumpa fursa jaji kuweza kubaini iwapo uamuzi huo ulifaa kuchukuliwa ama iwapo unaweza kutengwa.