Uingereza yaipa Tanzania sh. Trilioni 1

Waziri wa Uingereza Rory Stewart, alipotembelea shule moja nchini Tanzania wakati wa ziara yake Haki miliki ya picha Tanzanian Daily News, Government newspaper
Image caption Waziri wa Uingereza Rory Stewart, alipotembelea shule moja nchini Tanzania wakati wa ziara yake

Uingereza imetoa msaada wa Dola za Marekani milioni 450 sawa na shilingi trilioni moja za Tanzania kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Waziri wa nchi anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa na Masuala ya Afrika katika ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuia ya Madola ya Uingereza, ametangaza msaada huo wakati wa ziara yake nchini Tanzania.

Amesema fedha hizo zitaelekezwa katika maeneo mbalimbali, hususan katika kuinua ubora wa elimu na kuongeza idadi ya watoto wanaopata elimu, kuimarisha miundo mbinu hasa barabara na bandari.

Fedha hizo pia zitatumika katika kuinua kilimo cha biashara na viwanda, hususan vya pamba na nyama.

Katika ziara yake pia amefanya mazungumzo na Rais wa Tanzania John Magufuli, ambaye alimpongeza kwa kazi inayofanywa na serikali yake katika mapambano dhidi ya rushwa na hatua zionazochukuliwa kuimarisha elimu kwa kuwapa nafasi Watanzani wengi zaidi kupata elimu.

Katika ziara hiyo Waziri huyo wa Uingereza alipata nafasi pia ya kutembelea shule moja jijini Dar es Salaam na kujionea sera ya kutoa elimu bila ya malipo, ilivyoleta mabadiliko katika kuongeza idadi ya wanafunzi.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameishukuru Uingereza kwa msaada unaolenga kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali yake.

Uingereza ndiyo nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania