Serikali yafuta leseni za Magazeti Tanzania

Miongoni mwa vigezo vya kupatiwa usajili ni pamoja na kuwasilisha nakala ya muundo wa chapisho wasifu wa Wahariri pamoja na Waandishi wa chapisho hilo Haki miliki ya picha Google
Image caption Miongoni mwa vigezo vya kupatiwa usajili ni pamoja na kuwasilisha nakala ya muundo wa chapisho wasifu wa Wahariri pamoja na Waandishi wa chapisho hilo

Magazeti na machapisho yote ya habari nchini Tanzania yatasajiliwa upya kuanzia tarehe 23 mwezi Agosti hadi Octoba 15 ,2017 ikiwa ni utekelezaji wa kifungu cha tano (e) cha Sheria ya Huduma za habari 2016.

Agizo hilo lilotolewa na Idara ya Habari Maelezo kupitia Mkurugenzi wake ambaye pia ni msemaji mkuu wa serikali Dr. Hassan Abbas, linayahusu magazeti na machapisho yote ya habari ambayo yalipatiwa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo tayari imefutwa.

Utoaji huo wa leseni pia ni kwa mujibu wa Kanuni ya 7 ya Kanuni za Sheria ya huduma za habari za mwaka 2017 zilizochapishwa kwa mujibu wa tangazo la serikali Na 18 la Februari 3, 2017

Agizo hilo pia linafungua milango kwa usajili wa machapisho mapya kwa kufuata utaratibu mpya baada ya zoezi la usajili kuwa limesitishwa kwa muda toka kuundwa kwa sheria mpya.

Miongoni mwa vigezo vya kupatiwa usajili ni pamoja na kuwasilisha nakala ya muundo wa chapisho wasifu wa wahariri pamoja na waandishi wa chapisho hilo, hii ikiwa ni kutilia mkazo kipengele cha wanahabari kuwa na elimu katika fani ya habari kwa ngazi ya stashahada.