Kamanda wa meli ya jeshi la Marekani iliogongwa afutwa kazi

Admirali Aucoin Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Admirali Aucoin

Jeshi la wanamaji nchini Marekani limemfuta kazi naibu admirali Joseph Aucoin kama kamanda wa wanamaji wa meli ya saba ya kijeshi kufuatia misururu ya kugongana ilioshirikisha meli za kivita barani Asia.

Mabaharia 10 wanagali hawajulikani waliko baada ya manuwari ya USS John S McCain kugongana na meli ya mafuta karibu na Singapore siku ya Jumatatu.

Maafisa wa jeshi la wanamaji wanasema kuwa mabaki ya watu yamepatikana katika sehemu kadhaa za meli hiyo ambayo sasa ipo katika bandari ya Singapore.

Ajali hiyo ilikuwa ya nne mwaka huu.

Katika taarifa yake , jeshi la wanamaji limesema limepoteza imani na uongozi wa naibu Admirali Aucoin.

Meli hiyo ya saba inayopiga kambi mjini Yokosuka nchini Japan , ndio kubwa zaidi ya Marekani iliotumwa nje ya taifa hilo ikiwa na manuwari kati 50 hadi 70.

Naibu Admirali Aucoin ambaye amekuwa kamanda wake tangu 2015 alitarajiwa kustaafu wiki chache zijazo.

Mrithi wake atachukua uongozi wa meli hiyo mara moja.

Kufutwa kwake ni hatua mojawapo zilizochukuliwa na wanamaji hao baada ya jali hiyo ilioshirikisha meli ya USS John S McCain.

Haijulikani iwapo kutakuwa na tangazo rasmi.

Kisa hicho kilisababisha kusimamishwa kwa operesheni za meli za wanamaji wa Marekani na kuangazia marekebisho ya operesheni hizo.