Tamasha lafutiliwa mbali Uholanzi kutokana na tishio la ugaidi

Gari lilipatikana katika barabara iliyo karibu na ukumbi huo Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Gari lilipatikana katika barabara iliyo karibu na ukumbi huo

Gari lililokuwa na mikebe ya gesi ya kutoa machozi limepatikana katika ukumbi ambapo kulipangiwa kufanyika tamasha ya muziki mjini Rotterdam nchini Uholanzi, saa chache baada ya tahadhari kutoka kwa polisi wa Uhispania kusababisha kufutiliwa mbali kwa tamasha hilo la muziki.

Dereva wa gari hilo lililosajiliwa nchini Uhispani amekamatwa na kuziliwa na polisi, meya wa mji wa Rotterdam Ahmed Aboutaleb amewaambia wanahabari.

Bendi kutoka Marekani ya Allah-Las, ambayo mara nyingi hupokeza vitisho kutokana na jina lake, ilikuwa imepangiwa kutumbuiza katika ukumbi wa The Maassilo.

Lakini tahadhari kutoka kwa polisi lilisababisha kufutiliwa mbali kwa tamasha hiyo dakika za mwisho.

Hata hivyo Bw Aboutaleb amesema haijabainika iwapo gari hilo lina uhusiano na tishio la shambulio la kigaidi.

Lakini tahadhari hiyo ya polisi wa Uhispania ilitolewa kukiwa na hali ya juu ya tahadhari baada ya mashambulio kadha kutekelezwa Uhispania wiki iliyopita.

Lakini maafisa wa mahakama wameambia shirika la habari la Reuters kwamba hakuna uhusiano wowote kati ya mashambulio hayo ya Uhispania na onyo kutoka kwa polisi wa Uhispania, ambalo inadaiwa limetokana na uchunguzi wa muda mrefu.

Polisi wa Uholanzi pia wamemkamata dereva wa gari hilo kutoka Uhispania na anahojiwa.

Kikosi cha kuchunguza na kutegua mabomu kimetumwa eneo hilo, taarifa zinasema.

Polisi waliovalia fulana zisizopenya risasi wamefika eneo hilo, baada ya watu wote kuamrishwa kuondoka.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mikebe ya gesi ya kutoa machozi ilipatikana kwenye gari karibu na eneo hilo

"Polisi walikuwa wamezingira eneo la ukumbi huo na hilo lilisaidia kupatikana kwa mikebe hiyo ya gesi," Bw Aboutaleb amesema.

Katika mashambulio ya wiki iliyopita katika jimbo la Catalonia nchini Uhispania, watu 15 waliuawa katika mashambulio Barcelona na katika mji wa Cambrils.

Mashambulio hayo yalitekelezwa baada ya mlipuko katika nyumba iliyokuwa imejaa mikebe ya gesi ambapo washambuliaji inadaiwa walikuwa wanaandaa vilipuzi zaidi.

Katika mahojiano mwaka jana, kundi hilo la muziki aina ya Rock la Allah-Las liliambia gazeti la Guardian la Uingereza kwamba huwa linapokea vitisho mara kwa mara kutoka kwa Waislamu ambao hukerwa na kutumiwa na neno Allah - Mungu kwa Kiarabu - kama jina lake.

Kundi hilo lilisema lilitaka kuwa na jina lenye sifa za kidini baada ya kuhamasishwa na kundi jingine liitwalo Jesus and Mary Chain.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii