Melania Trump amshukuru Chelsea Clinton kwa kumtetea mwanawe Barron

Barron, Melania na Donald Trump White House, 11 June Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Melania Trump na mwanawe Barron walipokuwa wanahamia White House mwezi Juni

Mke wa Rais wa Marekani Donald Trump, Melania, amemshukuru binti wa mgombea urais aliyeshindana na Bw Trump katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana Chelsea Clinton kwa kumtetea mwanawe.

Bi Clinton aliandika kwenye Twitter akimuunga mkono Barron Trump, 11, baada ya tovuti moja ya habari kukosoa mavazi yake.

Bi Trump alimjibu kwenye Twitter kwa kuandika: "Asante @ChelseaClinton - ni muhimu sana kuwasaidia watoto wetu katika kuwawezesha kujiendekeza!"

Kichwa cha habari cha tovuti ya Daily Caller Jumatatu kilikuwa kinasema: "Wakati umefika kwa Barron Trump kuanza kuvalia kama mtu aliye White House."

Watu wengi katika mitandao ya kijamii walikubaliana kwamba taarifa hiyo ilivuka mipaka.

"Sawa na katika serikali za awali, tunawaomba wanahabari wamwache Barron na kuheshimu maisha yake ya faraghani," msemaji wa Bi Trump, Stephanie Grisham, aliambia shirika la Associated Press.

"Yeye bado ni mtoto na ana haki ya kuishi maisha yake ya utotoni kwa faragha."

Bi Clinton, aliyeishi katika White House babake alipokuwa rais wa Marekani miaka ya 90, aliandika kwenye Twitter: "Wakati umefika kwa wanahabari na kila mmoja kumwacha peke Barron Trump na kumwacha aishi maisha ya faragha ya utotoni anayostahiki."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Chelsea Clinton aliishi sehemu ya maisha yake ya utotoni ikulu

Aidha, alimjibu mmoja wa watu waliosambaza taarifa hiyo ya Daily Caller na kumwambia: "Hakuna mtoto yeyote tule anayefaa kuzungumziwa kwa njia kama hii katika maisha halisi au hata mtandaoni. Na kwa mtu mzima kufanya hivyo? Kwa aibu".

Bi Clinton amewahi kumtetea Barron awali aliposhutumiwa na kukosolewa na hata kufanyiwa utani.

Wakati mmoja, aliandika ujumbe ambao ulisababisha mtangazaji wa kipindi cha runinga cha Saturday Night Live kufutwa kazi.

Donald Trump alizoea kumshambulia Hillary Clinton kwa maneno walipokabiliana katika uchaguzi wa urais mwaka 2016, mara nyingi akimwita "crooked Hillary" maana yake 'Hillary mwovu'.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Melania Trump alikuwa awali amesema jamii imekuwa katili sana kwa watoto

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii