Serikali Kenya yasisitiza marufuku ya mifuko ya plastiki itatekelezwa

Karatasi za plastiki
Image caption Karatasi za plastiki za zapigwa marufuku nchini Kenya

Serikali ya Kenya imesisitiza kwamba marufuku ya mifuko ya plastiki, ambao imepangiwa kuanza kutekelezwa Jumatatu itatekelezwa kama ilivyopangwa.

Kenya kwa mara ya pili inajaribu kujiunga na mataifa mengine kwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia utengenezaji wake, uuzaji na utumiaji wa mifuko hiyo.

Serikali ilitangaza rasmi mpango wa kupiga marufuku mifuko hiyo Februari mwaka huu.

Kulingana na waziri wa mazingira nchini humo, Prof Judy Wakhungu mazungumzo kuhusiana na karatasi hizo yalianza miaka 15 iliyopita licha ya kwamba shirikisho la muungano wa watengenezaji wa bidhaa Kenya linaomba kupewa muda zaidi kutafuta njia mbadala.

Prof Wakhungu, amesema sababu kuu ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki ni uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mifuko hiyo.

"Kila Mkenya kikatiba ana haki ya kuwa na mazingira safi ili asipate matatizo ya kiafya yanayotokana na mifuko ya plastiki," amesema.

Akizungumza na gazeti la Daily Nation amewasihi Wakenya kuchukua jukumu lao binafsi kuhakikisha wanapata mazingira bora.

Kulingana na utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira, iwapo matumizi ya plastiki yataendelea kutumiwa ifikapo mwaka 2050 kutakuwa na viwango vikubwa vya plastiki kwenye bahari kuliko samaki.

Shirika la Usimamizi wa Mazingira Kenya (NEMA) imetoa onyo kali kwa wachuuzi, kampuni za utengenezaji wa mifuko hiyo na hata wale wanaouza mifuko hiyo nchi za nje kuzingatia sheria hiyo ifikapo Agosti 28.

Kulingana na utafiti uliofanywa na NEMA, wakiwashirikisha Umoja wa Mataifa karatasi za plastiki milioni 100 hutumiwa nchini Kenya na maduka ya jumla pekee.

Hata hivyo licha ya marufuku hiyo, kuna aina ya karatasi hizo za plastiki zilizosazwa kama zile zinazotumika kwa kampuni kupakia bidhaaviwandani na karatasi hizo zitapatikana tu kwa kampuni hizo na wala hazitauzwa madukani.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mifuko ya plastiki
Image caption Wakenya wameshauriwa kutumia mifuko mbadala

Mifuko ya kubebea taka haijajumuishwa katika marufuku hiyo lakini kampuni zinazotengeneza mifuko hiyo zinastahili kuweka jina la kampuni inayozitengeneza na atakayetumia mifuko hiyo kwenye mifuko hiyo

Serikali imewahimiza watu kutafuta mbinu mbadala za kubebea mizigo yao.

Tarehe 28 mwezi Agosti yeyote atakaye enda kinyume cha sheria hiyo anawezwa kutozwa faini ya kati ya shilingi milioni mbili na milioni nne pesa za Kenya (Dola 20,000-40,000 za Marekani) ama kifungo cha kati ya mwaka mmoja na miaka minne gerezani, au adhabu zote mbili.

Serikali ilikuwa imetoa muda wa miezi sita tangu Februari kwa kampuni kujiandaa kwa mabadiliko hayo na imesisitiza kwamba haitaongeza muda wake.

Kenya inajiunga na nchi nyingine za Afrika kama vile Mali, Mauritania, Tanzania, Uganda, Afrika Kusini na Rwanda katika kuchukua hatua kupiga marufuku mifuko ya plastiki.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii