Yingluck: Mahakama yatoa kibali waziri mkuu wa zamani Thailand akamatwe

Bangkok, Thailand, 25 August 2017. Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mamia ya wafuasi wa Bi Yingluck walifika nje ya majengo ya mahakama ya juu Bangkok

Mahakama ya Juu nchini Thailand imeahirisha kikao cha kutoa hukumu katika kesi ambapo waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Yingluck Shinawatra ameshtakiwa makosa ya uhalifu ya kuzembea kazini.

Majaji hao wakiwa mjini Bangkok wametoa kibali cha kukamatwa kwake wakisema hawaamini alivyosema kwamba amekosa kufika mahakamani kwa sababu anaugua.

Mahakama imeahidi kutoa huku tarehe 27 Septemba.

Ijumaa, mawakili wa Bi Yingluck waliomba hukumu icheleweshwe na kuambia mahakama kwamba anaugua kizunguzungu na hawangeweza kufika kortini.

Lakini taarifa rasmi ya Mahakama ya Juu imesema waendesha mashtaka "hawaamini mshtakiwa ni mgonjwa kwani hakuna cheti chochote cha matibabu kilichowasilishwa kwa mahakama, na kwamba hali yake ya afya si mbaya mno kiasi kwamba hawezi kufika kortini."

Mahakama imesema itatoa kibali cha kukamatwa kwake kwani anaweza kuikimbia nchi hiyo, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Kadhalika, mahakama imetwaa dhamana ya $900,000 (£703,000) ambayo alikuwa ameiweka wakati wa kuanza kwa kesi hiyo.

Bi Yingluck, amekanusha makosa ya kuzembea kazini yanayohusiana na mradi wa mpunga wa gharama ya mabilioni ya dola.

Iwapo atapatikana na hatia, anaweza akafungwa jela na pia kupigwa marufuku kutoshiriki siasa maishani yake yote.

Bi Yingluck, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Thailand mwaka 2011, aliondolewa madarakani mwaka 2015.

Kesi dhidi yake iliwasilishwa na serikali inayoungwa mkono na jeshi ambayo ilimuondoa mamlakani.

Lakini bado ni maarufu na anaungwa mkono sana.

Mamia ya wafuasi wake walikusanyika nje ya Mahakama ya Juu mjini Bangkok kabla ya kusomwa kwa hukumu dhidi yake, huku polisi wengi wakishika doria nje ya mahakama hiyo.

Mpango wa Bi Yingluck wa kulipia sehemu ya gharama ya mpunga ulikuwa sehemu ya ahadi zake kuu kwenye kampeni yake ya kutaka kuchaguliwa, na aliuzindua mwaka 2011 muda mfupi baada yake kuingia madarakani.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mradi huo wa mpunga ulikumbwa na utata wakati wa utawala wa Bi Yingluck

Lengo la mpango huo lilikuwa kuimarisha mapato ya wakulima na kusaidia kupunguza umaskini mashinani.

Chini ya mpango huo, serikali iliwalipa wakulima karibu maradufu ya bei ya mpunga sokoni kwa mazao yao.

Lakini uliathiri sana uuzaji wa mpunga kutoka Thailand nje ya nchi na kusababishia taifa hilo hasara ya zaidi ya $8bn (£6.25bn).

Serikali pia ilibaki na shehena kubwa ya mpunga ambao haingeweza kuuuza.

Ingawa mpango huo ulikuwa maarufu sana kwa wafuasi wake mashinani, wapinzani waliupinga wakisema ulikuwa ghali sana na ulitoa fursa ya kutokea kwa ulaji rushwa.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi dhidi yake, Bi Yingluck alisema kwamba hakuhusika katika shughuli za kila siku za kuusimamia mradi huo.

Amesisitiza kwamba yeye ni mwathiriwa wa mateso ya kisiasa.


Yingluck na utata kuhusu mradi wa mpunga

Mei 2011- Yingluck Shinawatra achaguliwa Waziri Mkuu, na muda mfupi baadaye anaanzisha mpango wa kufadhili kilimo cha mpunga

Januari 2014 - Maafisa wa kupambana na rushwa Thailand wamchunguza Bi Yingluck kuhusiana na mradi huo

Mei 2014 - Ashurutishwa kung'atuka baada ya mahakama ya kikatiba kumpata na hatia ya kutumia vibaya mamlaka katika kesi nyingine. Wiki chache baadake, jeshi lawaondoa maafisa wengine waliokuwa wake serikalini.

Januari 2015 - Bunge linaloungwa na jeshi lapitisha sheria ya kumuondoa Bi Yingluck madarakani kwa makosa ya ulaji rushwa kuhusiana na mradi huo wa mpunga, hatua inayompiga marufuku kutoshiriki siasa kwa miaka mitano. Aidha, anafunguliwa kesi.

Agosti 2017 - Bi Yingluck akosa kufika mahakamani wakati wa kutolewa kwa hukumu akisema anaugua.


Uongozi wa Bi Yingluck uligubikwa na utata pamoja na upinzani uliokuwa na nguvu.

Yeye ni dada mdogo wa tajiri na waziri mkuu wa zamani wa Thaksin Shinawatrwa na alikuwa akitazamwa na wapinzani wake kama kikaragosi wa kakake ambaye aliondolewa madarakani na jeshi mwaka 2006.

Lakini wawili hao bado ni maarufu sana miongoni mwa maskini mashinani, ingawa wanashukiwa sana na wakazi wa miji na watu wa mapato ya wastani.

Chama chao cha Pheu Thai kimekuwa kikishinda uchaguzi tangu 2001.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii