Mwanamke ajishindia $758m kwenye jackpot Marekani

Mavis Wanczyk

Mshindi wa pesa nyingi zaidi kuwahi kujishindiwa na mtu binafsi katika shindano la bahati nasibu Amerika Kaskazini - jumla ya $758.7m (£590m) - amejitokeza kuchukua zawadi yake, na ni mwanamke.

Mavis Wanczyk, 53, mama wa watoto wawili, alinunua tiketi yake ya ushindi katika kituo cha mafuta Chicopee, Massachusetts.

Mshindi huyo, ambaye namba zake za bahati zilikuwa 6, 7, 16, 23 na 26, na 4 - ameambia wanahabari kwamba tayari ameacha kazi.

Zawadi ya juu zaidi ya jackpot katika shindano la bahati nasibu ya kampuni ya US Powerball kuwahi kutolewa ilikuwa $1.6bn, lakini ilienda kwa washindi watatu ambao waligawana pesa hizo Januari 2016.

Wasimamizi wa mashindano ya bahati nasibu jimbo la Massachusetts waliambia wanahabari kwamba tiketi ya mwanamke huyo ambayo ilishinda Jumatano imethibitishwa kuwa halisi.

"jambo ninalotaka kufanya kwa sasa ni kuketi na ktuulia," alisema Bi lWanczyk.

Haki miliki ya picha WBZ-TV)
Image caption Tiketi ya ushindi ilinunuliwa katika kituo hiki cha mafuta Chicopee, Massachusetts

"Ni ndoto kuu ambayo imetimia."

Amewaambia wanahabari kwamba alichagua namba zake kwa kutumia tarehe za kuzaliwa za jamaa zake.

Bi Wanczyk, kuhusu kazi yake aliyoifanya kwa miaka 32 katika kituo cha matibabu, amesema: "Niliwapigia simu na kuwaambia sitafika tena kazini."

Aliongeza kwamba "nitaenda na kujificha kitandani mwangu".

Waandishi walimwuliza iwapo anapanga kujizawadi kwa vitu vizuri, mfano gari la kifahari.

Lakini Bi Wanczyk amejibu kwamba alinunua gari jipya chini ya mwaka mmoja uliopia, kwa mkopo, na sasa anapanga kulipa kiasi kilichosalia.

Afisa mmoja wa mashindano ya bahati nasibu laimweleza mwanamke huyo kama "mkazi wa kawaida sana wa Massachusetts".

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Watu wakisubiri kununua tiketi za bahati nasibu Hawthorne, California

Aliongeza kwamba anaonekana kama mwanamke mwenye bidii sana na kwamba bila shaka ana furaha isiyo na kifani.

Mwenye kituo cha petroli cha Pride, kilichopokea zawadi ya $50,000 inayotolewa kwa duka linalouza tiketi ya ushindi Bob Bolbuc amesema atatoa pesa hizo kwa hisani.

Malipo ya zawadi hiyo ya Jackpot, ambayo yanaweza kufanywa kwa awamu mara 29 kwa mwaka, au mara moja, yanakadiriwa kuwa karibu $443m baada ya kutozwa ushuru.

Mwenyekiti wa kampuni ya Powerball Charlie McIntyre amesema kupitia taarifa kwamba kuna tiketi nyingine sita - zilizouzwa Connecticut, Illinois, Louisiana, New Mexico, Pennsylvania na visiwa vya Virgin Islands - ambapo kila mmoja alishinda $2m.

Tiketi nyingine zilishinda $1m.

Maafisa wa mashindano ya bahati nasibu Massachusetts awali walisema tiketi hiyo iliuzwa Watertown, Boston lakini baadaye wakasahihisha hilo Alhamisi asubuhi.

Haijabainika kosa hilo lilitokea vipi.

Uwezekano wa kushinda jackpot hiyo ulikuwa moja kati ya 292.2 milioni.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii