Polisi wachunguza mlipuko wa Jumba la IMMMA mjini Dar es Salaam

Polisi wachunguza mlipuko wa Jumba la IMMMA mjini Dar es Salaam
Image caption Polisi wachunguza mlipuko wa Jumba la IMMMA mjini Dar es Salaam

Polisi mjini Dar es Salaam nchini Tanzania mapema siku ya Jumamosi wamesema kuwa wanaendelea kuchunguza kiwango cha mlipuko uliokumba kampuni moja maarufu ya mawakili katika shambulio la usiku.

Kamanda anayeondoka wa maeneo maalum mjini Dar, Bwana Lucas Mkondya aliambia gazeti la The Citizen nchini humo kwamba ni mapema mno kuweza kubaini kiwango cha mlipuko huo wa jumba la IMMMA.

''Sisi maafisa wa polisi tunachunguza swala hili.Tayari tumelitenga eneo hilo'',alisema kamanda Mkondya akiongezea: uchunguzi utakapokamilika tutakuwa na uwezo wa kusema ni nini kilichosababisha mlipuko huo.

Amesema kwamba kufikia sasa hakuna mtu aliyetiwa mbaroni kufuatia kisa hicho.

Shahidi mmoja wa kampuni hiyo amesema kuwa afisi hizo ziliharibiwa lakini hakuna kitu kilichoibwa.

''Wacha tuwaachie polisi wafanye uchunguzi wao'' , alisema wakili Magai.

Jumba la IMMMA lililopo katika eneo la Upanga katika barabara ya Umoja wa Mataifa lilikumbwa na mlipuko mwendo wa saa nane alfajiri.

Fatma Karume wakili maarufu na mwana wa aliyekuwa rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo.