Mambo 42 aliyoyafanya Donald Trump wakati wa likizo majira ya joto Marekani

President Donald J. Trump arrives at the The White House on the presidential helicopter

Wiki hii kote nchini Marekani na katika mataifa mengi duniani, watoto wanajiandaa kurejea shuleni kwa muhula mwingine. Inatarajiwa kwamba wengi watarejea nyumbani wakiwa na kazi ya ziada ya kuandika insha kuhusu mambo waliyoyafanya likizoni.

Rais wa Marekani Donald Trump mwenyewe amekuwa likizoni.

Sasa, chukulia kwamba wewe ni Donald Trump na umepewa kazi hiyo. Twafikiri jambo la kwanza utafanya ni kuomba karatasi ya ziada kwani umefanya mengi sana likizoni.

Kwenye mambo yako, huwezi kukosa kuyajumuisha haya ambayo wewe kama Trump na wenzako White House mmekuwa wakifanya, ambayo ni yafuatayo:

 • Alimwajiri mkurugenzi mpya wa mawasiliano kwa jina Anthony Scaramucci
 • Mkuu wake wa mawasiliano na wanahabari Sean Spicer ajiuzulu. Alisema anafurahia hatua hiyo lakini alionekana mwenye hasira
 • The Mooch (aka Scaramucci) alifanya mahojiano yasiyo ya kuridhisha na jarida la New Yorker
 • Trump amfuta mkuu wake wa utumishi wa umma Reince Priebus (ambaye aliachwa kambi ya jeshi la wanahewa ya Andrews)
 • Amwajiri mkuu mpya wa utumishi wa umma, Jenerali Kelly, ambaye alikuwa mkuu wa usalama wa ndani
 • Siku ya kwanza ya Kelly kazini, rais alimfuta kazi mkurugenzi wake mpya wa mawasiliano - Scaramucci aliyekuwa kazini siku 10 pekee.
 • Amwajiri mkurugenzi mpya wa mawasiliano, wa nne katika miezi saba.
 • Anamwaibisha hadharani mwanahesria wake mkuu, mara kadha, lakini Jeff Sessions anaendelea kuvumilia
 • Mswada wake wa huduma ya afya unashindwa bungeni
 • Anawashutumu hadharani wanachama watatu wa Republican waliopinga mswada huo, mara kadha
 • Apiga marufuku watu waliokumbatia jinsia tofauti kuhudumu jeshini, kupitia Twitter, bila kufahamisha jeshi
 • Wakuu wa jeshi wamwambia: "Sahau, huwa hatupokei amri kupitia Twitter; kuna njia ya mawasiliano"
 • Atoa hotuba ya kisiasa kwa maskauti wa miaka 11-18
 • Adai kiongozi wa maskauti alimpigia simu kumpongeza kwa hotuba njema zaidi aliyowahi kuitoa
 • Kiongozi wa maskauti asema hakumpigia simu kama hiyo, na kutoa taarifa kuwaomba radhi maskauti kwa sababu ya tamko hilo la rais
 • Asema rais wa Mexico alimpigia simu kumpongeza kwa sera zake kuhusu mpaka
 • Rais wa Mexico asema hakupiga simu kama hiyo
 • White House yakanusha kwamba rais ni mwongo, lakini yashindwa kufafanua kuhusu madai ya rais
 • Achukua siku nyingi kutia saini mswada wa vikwazo dhidi ya mataifa mengine (ikiwemo Urusi) na kisha alaumu bunge la Congress kwa kufanya autie saini
 • Amshukuru Vladimir Putin kwa kuwatimua mamia ya wanadiplomasia wa Marekani
 • Ashutumu wanaovujisha siri za Marekani lakini asema anapenda kuvujishwa huko kwa sababu humfanya watu wampende
 • Awahimiza polisi wawe wakati wakati wanapokuwa wakiwakamata washukiwa
 • Wakuu wa polisi washutumu taarifa hiyo. White House wafafanua kwamba ulikuwa mzaha
 • Amuaibisha hadharani kiongozi wa chama cha Republican katika bunge la Senati, ambaye anamhitaji sana ili mambo mengi yake yapitishwe, mara kadha.
 • Aonekana kuijibu Korea Kaskazini kwa kutishia vita vya nyuklia
 • Awaambia wakazi wa kisiwa cha Guam, ambacho kina kambi kubwa ya kijeshi ya Marekani, ambacho Korea Kaskazini ilikuwa imetishia kushambulia, kwamba hilo litasaidia utalii
 • Mkuu wake wa mikakati Steve Bannon atoa tamko la kukinzana. Asema: "Hakuna mpango wowote wa kuingilia kijeshi Korea Kaskazini"
 • Atishia Venezuela kwamba anaweza kutumia jeshi kuingilia kati
 • Baada ya mkutano wa watetezi wa ubabe wa wazungu, ambapo mwanamke mmoja aliuawa, rais alaumu pande zote mbili
 • Baada ya kushutumiwa sana, ajirekebisha. Awashutumu watetezi wa ubabe wa wazungu, wafuasi wa siasa za Nazi na wanachama wa kundi la Ku Klux Klan
 • Huku akiwa na hasira kwa sababu ya kulazimishwa kujirekebisha, abadilisha mambo na kurejelea kulaumu pande zote mbili na kusema kwamba kuna watu wazuri katika makundi yote.
 • Wakuu wa jeshi watoa taarifa ambapo walishutumu aina zote za ubaguzi, katika hatua iliyoonekana kama kumshutumu amiri jeshi mkuu
 • Apigia debe shaba lake la mizabibu Virginia alipoulizwa iwapo yeye - kama rais - atazuru Charlottesville
 • Hatua iliyomfanya kushutumiwa na viongozi wa Democrat, Republican, marais wa zamani, viongozi wa nchi nyingine duniani, washirika wake, wafanyakazi wake na hata Papa Francis mwenyewe.
 • Awadhalilisha hadharani wakuu wa kampuni waliokuwa wakijitenga naye. Wakuu watendaji wengine wa kampuni waondoka kwenye baraza lake la washauri muhimu White House
 • Amfuta kazi Steve Bannon, mkuu wake wa mikakati ambaye alikuwa mkuu wake wa kampeni na aliyesaidia sana ushindi wake
 • Apiga 'U-turn' kuhusu Afghanistan na kuahidi kutuma wanajeshi zaidi, bila kujali kwamba alikuwa awali amesema mara nyingi kwamba angeondoa majeshi ya Marekani nchini humo
 • Atishia kuifunga serikali iwapo hatapata ufadhili wa ujenzi wa ukuta mpaka wa Marekani na Mexico
 • Awaomba watu wa Marekani kuonyesha umoja
 • Siku iliyofuata, washutumu vikali maadi na wakosoaji wake katika hotuba iliyowagawanya wengi
 • Siku moja baadaye, ahimiza umoja
 • Amsamehe liwali wa zamani wa Arizona Joe Arpaio, aliyekuwa amepatikana na kosa la kukaidi agizo la mahakama kwamba asitishe doria barabarani dhidi ya wahamiaji haramu.

Mkuu wa utumishi wa umma wa zamani wa Barack Obama ambaye sasa ni meya wa Chicago, Rahm Emanuel, wakati mmoja aliandika kwenye Twitter kwamba atapendekeza White House itunukiwe tuzo ya sanaa ya Tony kwa kuwa na hadithi ya kuchekesha zaidi.