Mzozo wa Korea Kaskazini na Marekani kwa muktasari

Image from North Korean media of four missile launches on 7 March 2017

Chanzo cha picha, Reuters

Mzozo unaohusisha Korea Kaskazini ni mzozo ambao unaweza hata kusababisha vita vya vinyuklia, vita ambavyo huenda pengine haviwezi vikawa na mshindi. Lakini ni mzozo wenye mambo mengi tata. Hebu tuchanganue kiasi.

Ni kwa nini Korea Kaskazini inataka silaha za nyuklia?

Rasi ya Korea iligawanyika na kuwa mataifa mawili baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kukawa na Korea Kaskazini na Kusini. Korea Kaskazini iliegemea siasa za Kikomunisti na iliongozwa na serikali ya kiimla, uongozi sawa na wa Stalin katika Muungano wa Usovieti. Marafiki wake wakuu ni Urusi na Uchina.

Nchi hiyo ilijitenga pakubwa na nchi nyingine, isipokuwa nchi kadha marafiki wake. Viongozi wa nchi hiyo wanasema silaha za nyuklia ndiyo njia pekee ya kujikinga dhidi ya maadui kutoka nje ambao wanataka kuliangamiza taifa hilo.

Wamekaribia kiasi gani?

Majaribio yake ya karibuni zaidi ya makombora yanaachilia kwamba nchi hiyo inakaribia sana kuwa na makombora ya kuruka kutoka bara moja hadi jingine yanayofahamika kama (ICBM) ambayo yana uwezo wa kufika Marekani bara.

Wamefanyia majaribio silaha za nyuklia mara tano. Taarifa za kijasusi zinadokeza kwamba nchi hiyo inakaribia sana, au tayari imeweza, kuunda kichwa kidogo cha silaha za nyuklia kinachoweza kuwekwa kwenye makombora.

Nchi hiyo inaichukulia Marekani kuwa adui wake mkuu na pia ina maroketi ambayo yameelekezwa kwa Korea Kusini na Japan, nchi ambazo zina wanajeshi wengi sana wa Marekani.

Nini kimefanywa kuwazuia?

Juhudi za kutumia mashauriano kutatua mzozo huo zimeshindwa kupata suluhu kufikia sasa.

Umoja wa Mataifa umeiwekea nchi hiyo vikwazo vingi - lakini bila mafanikio.

Uchina, mshirika wake wa dhati, pia imeiwekea shinikizo za kiuchumi na kidiplomasia.

Marekani sasa imetishia kutumia nguvu za kijeshi na Rais Donald Trump awali aliitahadharisha kwamba itakabiliwa kwa "moto na ghadhabu".

Lakini kwa muda sasa uhasama unaonekana kupungua na mazungumzo kati ya Bw Trump na Bw Kim yamepangwa kufanyika 12 Juni nchini Singapore, ingawa Korea Kaskazini imetishia kujiondoa.

Marekani inaweza kuishambulia Korea Kaskazini?

Mzozo huo umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi, lakini hali kwamba Korea Kaskazini inakaribia kuwa na/ au tayari ina uwezo wa kuunda kichwa kidogo cha nyuklia kinachoweza kuwekwa kwenye makombora, na kwamba ina makombora yanayoweza kufikia Marekani bara, yanabadilisha mambo sana.

Miezi kadha mwaka uliopita, kulikuwa na hatua za 'uchokozi' mara kadha za Korea Kaskazini pamoja na majibizano kati yake na Marekani ambazo zimezidisha mzozo huo.

Korea Kaskazini ilitishia kurusha mabomu karibu na kisiwa cha Guam ambacho kinamilikiwa na Marekani katika Bahari ya Pacific.

Mwaka 2017 nchi hiyo imerusha kombora kupitia anga ya Japan.

Lakini huku majibizano yakiendelea, bado ni vigumu kubashiri ni nini kitafuata.

Septemba mwaka 2017 taifa hilo lilifanyia majaribio kombora la nyuklia ambalo lilisababisha tetemeko la ardhi la nguvu ya 6.3 kwenye vipimo vya Richter.

Maelezo ya picha,

Uwezo wa makombora ya Korea Kaskazini