Wabunge wa upinzani wakubali kula kiapo Kenya

Wabunge na maseneta wamekuwa wakifahamishwa kuhusu taratibu za bunge
Image caption Wabunge na maseneta wamekuwa wakifahamishwa kuhusu taratibu za bunge

Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance wametangaza kwamba wabungena maseneta wa muungano huo watahudhuria vikao vya kwanza vya Bunge la Taifa na Seneti Alhamisi siku ya Alhamisi.

Mabunge hayo mawili yanakutana kwa mara ya kwanza baada ya wabunge na maseneta wapya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti.

Shughuli ya kwanz Alhamisi inatarajiwa kuwa ya kuwalisha kiapo wabunge na maseneta.

Baadhi ya wabunge wa chama cha ODM ambacho ni mojawapo ya vyama vinavyojumuisha muungano wa Nasa walikuwa wametangaza kwamba wabunge wa muungano huo watasusia kikao hicho cha Bunge ambacho kimeitishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wabunge hao walidai Bw Kenyatta, ambaye ushindi wake umepingwa mahakamani na mgombea wa Nasa Raila Odinga hana mamlaka ya kuliita Bunge kwa vikao.

Leo hata hivyo, baada ya mkutano wa wabunge, maseneta na viongozi wa muungano huo, iliafikiwa kwamba wabunge hao na maseneta watahudhuria vikao hivyo na kula kiapo.

Mmoja wa viongozi wa Nasa Moses Wetangula aliambia kikao cha wanahabari baada ya kikao hicho kwamba wabunge hao wataenda kwa vikao hivyo "kuapishwa".

Wabunge na maseneta wanatarajiwa pia kuwachagua maspika na manaibu wao ambapo abadiliko kadha yanatarajiwa.

Chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta ambacho kina wingi wa wabunge na maseneta kimeafikiana umuunga mkono aliyekuwa gavana wa Bungoma Ken Lusaka kuhudumu kama spika wa bunge la Seneti.

Spika wa awali Ekwe Ethuro amesisitiza kwamba bado atawania wadhifa huo akisema ana uzoefu wa kutosha na amekuwa kwenye bunge hilo.

"Iwapo kifaa chako hakijavunjika, ya nini kukiondoa?" amejitetea.

Muungano wa upinzani Nasa unamuunga mkono Farah Maalim.

Spika wa Bunge la Taifa la 11 Justin Muturi anatarajiwa kuhudumu tena katika wadhifa huo Bunge la 12 baada ya kuidhinishwa na Rais Kenyatta na chama chake kuwa mgombea atakayeungwa mkono na chanma hicho.

Mada zinazohusiana