Askofu wa kanisa Katoliki awapa hifadhi wakimbizi 2,000 Waislamu nchini CAR

Walinda amani wa Umoja wa mataifa, wamekuwepo nchini humo tangu mwezi Aprili mwaka 2014 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Walinda amani wa Umoja wa mataifa, wamekuwepo nchini humo tangu mwezi Aprili mwaka 2014

Askofu mmoja wa kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Afrika ya Kati-CAR, amewapa hifadhi zaidi ya Waislamu 2,000, ambao wanaishi kwa hofu ya kushambuliwa na kundi moja kuu la wanamgambo Wakristo nchini humo.

Juan José Aguirre Munoz, anasema wakimbizi hao hawawezi kutoka katika uwanja wa kanisa hilo lililoko Kusini Mashariki mwa mji wa Bandassou.

Ameiambia BBC kwamba, maisha ya wakimbizi hao yamo ''hatarini'' kutoka kwa waasi wenye silaha wa kundi la Balaka.

Wiki iliyopita, afisa mkuu wa umoja wa mataifa wa kitengo cha utoaji msaada wa kibinadamu, alitoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea mauwaji ya kimbari.

Stephen O'Brien, amesema kuwa vurugu inazidi kuongezeka huku hali ikiwa mbaya zaidi nchini humo.

"Vurugu zinaongezeka na kuhatarisha hali ya usalama, huku kukiwa na uwezekano wa kutokea kwa maafa zaidi hata kuliko ilivyokuwa miaka minne iliyopia."

Ameongeza kuwa: "tahadhari ya awali ya kutokea kwa mauwaji ya kimbari ipo. Lazima hali hii ikabiliwe sasa na haraka iwezekanavyo," alisema O`Brien.

Jamhuri ya Afrika ya Kati, imeshuhudia ghasia na mapigano mabaya zaidi tangu mwaka 2013, wakati kundi kubwa la waasi wa kiislamu- Seleka lilipochukua utawala wa nchi hiyo, na kulaumiwa kuwa lilikuwa likiauwa watu wasio Waislamu.

Makundi ya kujilinda yaliyopewa jina Balaka yaliundwa lakini nayo pia yamelaumiwa kwa mauwaji ya kiholela.

Jina Balaka ni jina la mtaani linalomaanisha risasi, kwa hivyo jina la kikundi hicho lina maana kuwa "Wale wanaosimamisha risasi". Na kwa upande mwingine jina la Seleka, lina maanisha, "muungano" hiyo ni kutokana na kabila la Sango, lugha inayungumzwa pakubwa nchini humo.

Kundi moja lililo na silaha, linalokabiliana na lile la Balaka liliundwa, na limeshutumiwa kwa mauaji mabaya ya watu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii