Washukiwa watano walioshtakiwa mauaji ya Benazir Bhutto waachiliwa huru Pakistan

Bi Benazir Bhutto, alihudumu mihula miwili kama waziri mkuu wa Pakistan Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bi Benazir Bhutto, alihudumu mihula miwili kama waziri mkuu wa Pakistan

Mahakama maalum nchini Pakistan, imewaachia huru washukiwa watano, wanaodaiwa kuwa wanamgambo wa Taliban, kwa kupanga na kutekeleza mauwaji ya aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Bi Benazir Bhutto, mwaka 2007.

Majaji katika kesi hiyo wamesema kuwa, hakuna ushahidi dhidi yao, lakini wakafungwa jela washukiwa wengine wawili, kwa uzembe wa kuzuia kutokea kwa mauwaji hayo.

Mahakama pia imetangaza kumuondolea mashtaka pia aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Pervez Musharraf, ambaye pia alihusishwa katika kesi hiyo, kama mtoro aliyekimbia haki.

Bi Bhutto aliuwawa kwa shambulio la risasi na bomu mara baada ya kuhutubia mkutano wa kisiasa wa uchaguzi mkuu.

Jenerali Musharraf amekuwa akiishi uhamishoni baada ya kuikimbia nchi hiyo mwaka jana, ambapo mali yake iliyoko Pakistan ilitaifishwa na serikali.

Hajasema lolote kuhusiana na uamuzi wa hukumu hiyo, na siku zote amekuwa akikanusha kuhusika kwa vyovyote na mauwaji hayo.

Serikali yake inamlaumu kinara mkuu wa kundi la Taliban nchini Pakistani, Baitullah Mehsud, kuhusika na mauwaji hayo, lakini amekanusha.

Bwana Mehsud, aliuwawa katika shambulio la ndege ya Marekani isiyokuwa na rubani, mwaka 2009.

Bi Bhutto, ambaye aliuwawa mnamo Disemba ya mwaka 2007, alikuwa mtu mashuhuri katika siasa za Pakistan, na alihudumu mara mbili kama waziri mkuu wa Pakistan.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwaka 2010, inasema kuwa kifo chake kingezuiwa na kwamba serikali ya Bwana Musharraf ilishindwa kutoa ulinzi wa kutosha- wakati ambapo walinzi wake walipopuuzilia mbali ripoti hiyo huku wakiitaja kama "pakiti ya uongo".

Mada zinazohusiana