Marekani yaiamuru Urusi kufunga afisi zake za kibalozi

San Francisco Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jengo lililo na afisi za kibalozi za Urusi San Francisco

Marekani imeiamuru Urusi kufunga afisi zake za ubalozi katika mji wa San Francisco na afisi nyingine mbili za ziada za kibalozi kutokana na "hatua isiyofaa iliyochukuliwa" na Urusi, maafisa wa Marekani wamesema.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetangaza hatua hiyo baada ya Urusi kupunguza idadi ya wafanyakazi wa kibalozi wa Marekani wanaofaa kuwa nchini Urusi mwezi jana.

Uamuzi huo umechukuliwa katika "kuendeleza moyo wa usawa," wizara ya mambo ya nje imeongeza.

Kufungwa kwa afisi hizo za kibalozi San Francisco na afisi za ziada Washington na New York kunafaa kukamilishwa kufikia Jumamosi.

Ingawa wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema hatua hiyo ya Marekani imetokana na kupunguzwa "kusikostahiki na kwenye madhara" kwa maafisa wa kibalozi wa Marekani nchini Urusi, imedokeza pia kwamba inataka mzozo wa sasa ufikie kikomo.

"Ingawa kutaendelea kuwepo ukosefu wa usawa katika idadi ya maafisa wa kibalozi, tumeamua kuiruhusu Serikali ya Urusi kuendelea kuwa na afisi nyingine kadha za ziada ili kujaribu kupunguza kudorora kwa uhusiano wetu,2 wizara ya mambo ya nje imesema kupitia taarifa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii