Rais Kenyatta: Ni haki yangu kuikosoa mahakama

Rais Uhuru Kenyatta akifanya kampeni katika eneo la Kajiado nchini Kenya

Chanzo cha picha, facebook/Ikulu ya rais

Maelezo ya picha,

Rais Uhuru Kenyatta akifanya kampeni katika eneo la Kajiado nchini Kenya

Rais Uhuru Kenyatta ametetea hatua yake ya kuikosoa mahakama ya juu na jaji mkuu David Maraga kwa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais akisema ni haki yake kufanya hivyo.

Akizungumza katika kampeni za chama cha Jubilee katika kaunti ya Kajiado siku ya Jumanne, rais Kenyatta amesisitiza madai yake kwamba mahakama hiyo ya juu ilipuuzilia mbali haki ya wananchi ili 'kumfurahisha' mtu mmoja aliyemtaja kuwa mpinzani wake Raila Odinga.

''Nina hasira kwasababu nilikosewa.Walibatilisha uchaguzi wangu kimakosa.lazima tuseme ukweli'', alisema wakati wa kampeni za chama chake katika eneo la Kiserean.

Alisema kwamba licha ya kuwa anaheshimu uamuzi wa mahakama hiyo anajua kwamba alishinda uchaguzi huo kwa zaidi ya kura milioni 1.4.

Licha ya uamuzi huo bwana Kenyatta amesema kuwa ana imani atashinda tena.

Akiandamana na naibu wa rais William Ruto pamoja na viongozi wa chama tawala cha Jubilee, rais alisema kuwa hakuna kilichobadilika kwa kuwa Wakenya waliompigia kura watampigia kura kwa mara nyengine.

''Tulishinda kwa haki. Tulishinda kwa zaidi ya kura milioni 1.4, lakini mahakama ikaamua kutunyima ushindi wetu.Tuko tayari kwa uchaguzi mpya'', alisema bwana Kenyatta.