Tume ya uchaguzi Kenya yatetea uamuzi kuhusu tarehe ya uchaguzi mpya

Wafula Chebukati Haki miliki ya picha AFP/Getty

Tume ya taifa ya uchaguzi Kenya (IEBC) imetetea uamuzi wake wa kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi mkuu kuwa 17 Oktoba na kwamba ni wagombea wawili pekee wa urais watashiriki.

Tume hiyo, ambayo imeonekana kukumbwa na mgawanyiko miongoni mwa makamishna, hata hivyo imesema inatarajia mahakama itatoa mwongozo zaidi.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alisema uamuzi huo uliongozwa na uamuzi wa mahakama ya juu mwaka 2013 ambapo mahakama hiyo ilitoa ufafanuzi kuhusu maana ya "uchaguzi mpya".

Tume hiyo ilitangaza kwamba ni Rais Uhuru kenyatta pekee aliyekuwa ametangazwa mshindi mwezi uliopita lakini ushindi wake ukapingwa na mgombea wa upinzani Raila Odinga mahakamani, na Bw Odinga, ambao watashiriki uchaguzi huo.

Mmoja wa waliowania urais mwezi uliopita Dkw Ekuru Aukot wa chama cha Thirdway Alliance amefika kortini kupinga uamuzi wa tume hiyo.

"Tunafahamu kwamba kuna maswali yameibuliwa kuhusu ufafanuzi wa tume hii wa msimamo kuhusu suala hili kisheria. Kwa kuwa uamuzi wa tume umepingwa Mahakama ya Juu, tunatumai kwamba mahakama itatoa mwongozo zaidi," amesema Bw Chebukati.

Bw Odinga na muungano wake wa National Super Alliance (Nasa) walikuwa pia wamepinga kutangazwa kwa tarehe 17 Oktoba kuwa tarehe mpya ya uchaguzi.

Rais Kenyatta aishtumu mahakama kwa kubatilisha uchaguzi

Uhuru Kenyatta: Idara ya mahakama ina 'tatizo'

Rais Kenyatta: Ni haki yangu kuikosoa mahakama

Rais Kenyatta hata hivyo ameunga mkono uamuzi wa tume hiyo na kusema hakuna takwa la kisheria kwa tume hiyo kushauriana na vyama vya kisiasa na wagombea kabla ya kutangaza tarehe ya uchaguzi.

Tume hiyo imesema imetayarisha bajeti ya uchaguzi huo mpya na kuwasilisha kwa Hazina Kuu.

Tume hiyo imetoa wito kwa vya kisiasa kuhakikisha vimetuma maajenti "wenye uzoefu na waliojitolea kwa dhati" katika maeneo yote nchini.

"uchunguzi wa awali unaonesha kuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Agosti, vyama vya kisiasa havikuratibu vyema shughuli ya kutuma maajenti na katika baadhi ya vituo, hakukuwa na maajenti," amesema Bw Chebukati.

"Wagombea wanafaa wahakikishe maajenti wao wanafahamu vyema teknolojia itakayotumiwa na wakamilishe kutayarisha orodha ya maajenti katika vituo, ngazi ya eneo bunge na kituo cha taifa cha kujumlishia matokeo."

Tume hiyo imesema wasimamizi wa uchaguzi ambao waligunduliwa kuvunja sheria wakati wa uchaguzi wa mwezi uliopita hawatashirikishwa katika uchaguzi mpya.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii